Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya, amakutana na Madereva wa Halmashauri hiyo na kufanya kikaa kazi, chenye lengo la kukumbushana majukumu na kupata mrejesho wa kazi zinazotekelezwa na madereva hao katika Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Makwinya, amewataja Madereva kuwa ni injini ya Halmashauri kwa kuwa bila wao, Halmashauri haiwezi kufikia malengo yake, wakiwa na kazi kubwa ya kuwapeleka watalamu kwenye usimamizi wa Miradi ya maendeleo na utekelezaji wa kazi zote ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
"Nyinyi mnafahamu maeneo yote ya halmashauri, maeneo ambayo shughuli za halmashauri zinatekelezwa ikiwemo miradi ya maendeleo, mnavifahamu vyanzo vyote vya mapato pamoja na maeneo yote ya wananchi, nikitaka kupata taarifa mnaweza kunipa taarifa nzuri kwa kuwa kila wakati mnapita katika maeneo mbali mbali ya halmashauri" Amesema Makwinya.
Aidha, Mkurugenzi huyo licha ya kueleza namna anavyotambua kazi kubwa inayofanywa na madereva hao, amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya halmashauri na ya Serikali kwa ujumla wake kwa kuzingatia kanuni,sheria na taratibu za utumishi wa Umma kwa kuwa Serikali imewaamini na kuwakabidhi jukumu hilo.
Hata hivyo, katika kikao hicho, Mkurugenzi amewaalika wataalam kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kutoa elimu ya matumizi ya vyombo vya moto na namna ya kujikinga na Majanga.
Naye, Afande wa Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Arumeru, ASF. Kimaro ametoa elimu ya matumizi na usalama wa vyombo vya moto kama vile matumizi sahihi ya " Fire Extinguisher" pamoja na upimaji wa vyombo wanavyovitumia.
ASF Kimaro amewataka Madereva hao, kuwa na tabia ya kufanyia uchunguzi wa kiufundi magari wanayoyaendesha, ikiwa ni pamoja na kuyapeleka magari hayo kukaguliwa na Jeshi la Zimamoto.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa