Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wadau wa utalii wa vyakula kuwekeza zaidi katika kuandika vitabu vya vyakula vya Kiafrika na machapisho ya kuandaa mapishi ili kuongeza ujuzi na kupunguza woga kwa watalii wa matumizi ya vyakula wasivyovifahamu.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Utalii wa Vyakula Barani Afrika unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia Jijini Arusha. Amesema ni muhimu kutangaza kwa kiwango kikubwa vyakula vya kitamaduni vya Afrika ili utalii wa vyakula uweze kukua na kustawi.
Ameongeza kwamba kwa sasa watalii wengi hawana ufahamu wa utajiri wa Vyakula vya Kitamaduni vilivyopo Barani Afrika, vilevile ndani ya nchi za Afrika, utalii wa vyakula umewekwa kwa kiwango kidogo katika mikakati ya kitaifa ya maendeleo ya utalii.
Aidha Makamu wa Rais amesema katika kukuza utalii wa vyakula Barani Afrika inahitajika utengaji wa maeneo maalum na njia za kitamaduni ambapo bidhaa za ndani na vyakula vya kipekee vitatayarishwa kwaajili ya watalii kufurahia. Amesema katika njia na vituo hivyo vya chakula, ubora wa vyakula na bidhaa za asili ni lazima kudumishwa.
Ameongeza kwamba hivyo kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wapishi wa vyakula vya asili, wazalishaji wa ndani, waongozaji watalii na wadau wengine wa utalii ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa watalii ni endelevu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa