"Hakuna Mkulima atakaepatiwa pembejeo za kilimo kama hajasajiliwa kwenye mfumo".
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kujadili mwenendo wa zoezi la utambuzi na usaliji wa wakulima na usambazaji wa mbolea kwa Mkoa wa Arusha.
Amesema Mkulima asiposajiliwa mfumo wa usambazaji wa mbolea hautamtambua hivyo utasababisha kukosa mbolea.
Aidha, amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwenda kusimamia usajili wa wakulima hao na kutoa taarifa kila wiki Mkoani.
Serikali imeweka mfumo huo ili kupunguza hadha ambayo Mkulima alikuwa anaipata ikiwemo kucheleweshewa Mbolea na kusababisha hasara.
Mongella amesema zaidi ya 89% ya wakazi wa Arusha ni wakulima hivyo wanatakiwa wote watambulike kwenye mfumo.
Hadi sasa Mkoa ameweza kusajili wakulima 20,136 na wastani wa usajili kitaifa kila halmashauri isajili wakulima 2000 kwa siku.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amesema zoezi la usajili litaweza kukamilika ikiwa kutakuwa na ushirikiano kati ya watendaji wa Halmashauri na Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Kikao kazi hicho kilijumuisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmshauri, wataalamu na wadau wa Kilimo Mkoania Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa