Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bwana Richard Kwitega ameziagiza halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha zinafikia malengo ya asilimia 30 ya uwandikishaji wa bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha tathimini ya mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa kwa nusu mwaka Mkoani Arusha.
Amesema malengo ya Kitaifa ni kuhakikisha asilimia 30 ya kaya zinafikiwa na huduma hiyo, hivyo hata Mkoa wa Arusha unatakiwa kuhakikihsa malengo hayo yanafikiwa kwa ukamilifu.
Aidha, amewataka waratibu wa mfuko wa bima ya afya kuhakikisha wanawafuatilia kwa ukaribu wanachama wanaopata huduma hiyo katika vituo vya kutoa huduma ili kubainisha changamoto zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati.
Pia, amewataka wakurugezni wa halmashauri zote kuhakikisha vifaa vya uwandikishaji vinapatikana kwa haraka zaidi ili kuongeza kasi ya uwandikishaji.
Kwitega amesema bima ya afya iliyoboreshwa umelenga zaidi kutoa huduma za afya kwa wananchi hasa walioko kwenye mfumo wa ajira zisizo rasmi, ili kuwarahisishia kupata huduma za afya kwa urahisi.
Mratibu wa bima ya afya iliyoboreshwa bwana Denis Mgiye amesema, bima ya afya iliyoboreshwa ilianza rasmi Julai 1, 2019 hadi kufikia Julai 1, 2020 idadi ya kaya 7,557 zimeshajiunga na bima ukilinganisha na kaya 3,055 za mwaka 2019.
Amesema idadi hiyo imepelekea ongezeko la uwandikishaji kufikia asilimia 2 kimkoa na kushika nafasi ya 9 Kitaifa ukilinganisha na nafasi ya 23 kwa mwaka 2019.
Amesisitiza kuwa mpaka sasa wanufaika wa bima hiyo ya afya iliyoboreshwa kwa Mkoa wa Arusha ni watu 36,785 na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ikiwa imesaidia kulipia kaya 1,300 zilizopo katika eneo la hifadhi hiyo.
Denis amesisitiza kuwa, mpaka sasa kiasi cha fedha shilingi milioni 91 kimeshapelekwa kwenye vituo vya kutolewa huduma vya Mkoa wa Arusha.
Amesema changamoto kubwa ni baadhi ya maafisa uwandikishaji kutopeleka fedha beki na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa utoaji huduma kwa wanachama.
Pia,ukosefu wa vifaa vya uwandikishaji kwasababu ya baadhi ya halmashauri kutolipa madeni kwa wakati.
Amesema mpaka sasa Mkoa umeweka mikakati mbalimbali ikiwemo, kila Kijiji kuandikisha kaya zisizopungua 31 kwa mwezi,kuhakikisha halmashauri zinalipa madeni ya kununua vifaa vya uwandikishaji na kuendelea kuhamasisha jamii kujiunga na bima ya afya.
Kikao hicho cha tathimini kilikuwa na lengo la kubaini hali halisi ya mwenendo wa huduma hiyo ya bima ya afya iliyoboreshwa tangu ilipoanzishwa mnamo Julai 2019 na mpaka sasa ikiwa imefikisha mwaka mmoja.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa