Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema Msaada wa Kisheria unaotolewa bure kwa Wananchi wote wa Tanzania ni maono na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema dhamira ya Rais Samia ni kuona Haki za Binadamu zimetamalaki pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa Haki kwa kila Mwananchi.
Dkt. Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Machi 28, 2025 Jijini Arusha kwenye viwanja vya Ngarenaro, wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kusema kuwa, Haki za Binadamu ni pamoja na Haki za kiraia, kisiasa,kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
Waziri Ndumbaro amesisitiza kuwa katika Uongozi wake Rais Samia amekuwa kinara katika kuhakikisha Haki za kiuchumi zinakuwepo kwa kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kama alivyofanya kwenye filamu ya "The Royal Tour" sambamba na namna anavyoimarisha Haki za kijamii katika upatikanaji wa Elimu, Huduma za Afya, miundombinu na Huduma za maji safi na salama kwa Watanzania wote.
"Chimbuko la Msaada huu wa Kisheria ni maono ya Rais Samia na lilianza Januari 2023 na wakati ule Rais ananipigia simu kunipa maelekezo ya utekelezaji wake aliongozwa na Ilani ya CCM ibara ya 122 na sheria ya Msaada wa kisheria ya mwaka 2017 ambapo ilitakiwa elimu na Msaada wa Kisheria kutolewa kwa Wananchi wote ili kuondoa migogoro kwenye jamii." Amesema Waziri Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndumbaro ameeleza kuwa Arusha imepata upendeleo wa pekee kutokana na mapenzi makubwa ya Rais Samia kwa wakazi wa Arusha, kwa kuwa Mkoa ambao umefikiwa mara mbili ndani ya mwezi mmoja na timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa ubunifu, uchapakazi na kujitoa kwake kwa Wananchi, akiwataka Wananchi wa Mkoa wa Arusha kutobabaishwa na wanaokuja kwao nyakati za kampeni za kisiasa pekee.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa