"Watumishi tutaenda kuwajibika katika majukumu yetu na kuwapa ushirikiano mkubwa ili tulete maendeleo katika Mkoa wetu".
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella alipokuwa akizungumza kwenye kongamano la viongozi wa dini na kijamii la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, Katika kituo cha Mikutano AICC Jijini Arusha.
Amesema yote yaliyozungumzwa na viongozi hao yamesaidia katika kuonesha namna ya kuwakumbusha majukumu yao.
Aidha, amewahakikishia viongozi hao kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwao na kudumisha amani ya Mkoa.
Nae, Mwenyekiti Msaidizi wa Jumuiya ya Maridhiano Taifa Askofu Dkt.Israel Maasa amesema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kumuunga Mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa alizozifanya katika kuboresha maslahi ya watumishi hao.
Juhudi anazozionesha Mhe. Rais ni kutokana na utiifu kwa Mungu alionao ambao umemsaidia kuendesha nchi kwa amani.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa wa Arusha Shaban Bin Jumaa amesema kitendo Cha Rais Samia kukutana na vyama vya siasa hasa vya upinzani kumeonesha mashirikiano wa hali ya juu kwa maslahi ya Taifa.
Nae Kiongozi Mkuu wa kimila kutoka kabila la Maasai Laigwanan Ole Kisongo amewataka viongozi wa Mkoa wafanye kazi kwa uwaminifu, amani na mshikamano.
Amesema Rais Samia ni kiongozi wa kujenga mahusiano hivyo wamuunge Mkono kwa ujasiri zaidi kwani ameweza kuondoa michango ya ujenzi kwa wananchi.
Kongamano la viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano limefanyika maalumu la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mazuri aliyoyafanya ikiwemo uzinduzi wa filamu ya Royal Tour inayoenda kukuza utalii kwa Mkoa, ujenzi wa vyumba vya Madarasa na vituo vya afya na hasa juhudi za kumalizia miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali ya awamu ya Tano.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa