“Athari za lishe duni kwa watoto ndani ya siku 1000, madhara yake huwa yanatokea kwenye maisha yake yote”.
Yamesemwa hayo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega,alipokuwa akifungua kikao cha tathimini ya lishe cha nusu mwaka kwa Mkoa wa Arusha.
Amesema madhara ya lishe duni huwa ni makubwa sana kuliko jamii inavyoelewa hasa kwa watoto wadogo na wajawazito.
Ametaja baadhi ya athari hizo kuwa ni udumavu, kuvimba tezi la shingo, upungufu wa damu, upungufu wa madini ya chuma mwilini hasa kwa wajawazito na kupata vidonda mdomoni.
Amesema serikali ya awamu ya tano imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha hali ya lishe nchini inaimarika kwa kiwango kikubwa ili kuiwezesha nchi kuingia katika uchumi wa kati.
Kwitega amesisitiza kuwa ili hali ya lishe katika mkoa wa Arusha iweze kuimarika zaidi elimu itolewa kuanzia ngazi ya familia kupitia kwa waratibu wa lishe wa jamii.
Hivyo amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanatenga shilingi 1000 kwa kila mtoto wa chini ya umri wa miaka 5, ili fedha hizo zikasaidie kuongeza utoaji wahuduma za lishe katika ngazi zote.
Nae, afisa lishe Mkoa wa Arusha bi.Anna Andrew, amesema hali ya udumavu katika mkoa wa Arusha imeshuka kutoka asilimia 36 mwaka 2014 hadi asilimia 25.5 mwaka 2018 sawa na Watoto 75,959 walio katika mpango wa siku 1000 za lishe bora.
Amesema katika darasa lenye watoto 45 watoto 14 wana udumavu hivyo kupelekea kushindwa kufundishika.
Aidha, amesema changamoto kubwa inayosababisha hali ya udumavu kuendelea kuwepo katika Mkoa ni elimu duni kwa watoa huduma za lishe ngazi ya jamii na baadhi ya jamii kutowaibua watoto wenye udumavu.
Akitoa mikakati ya kupunguza udumavu katika Mkoa wa Arusha, Mganga Mkuu wa Mkoa Daktari Wedson Sichalwe, amesema mkoa utaendelea kusimamia hali ya lishe kwa wamama wajawazito na watoto kwa ukaribu zaidi, huku wakitoa elimu ya kutosha kwa watoa huduma za lishe ngazi zote.
Pia,Kutoa matibabu kwa wagonjwa watakaogundulika na ukondefu mkali na kuendelea kuhamasisha jamii kutumia chumvi ya madini joto ili kuongeza madini mwilini zaidi.
Kikao cha tathimini cha lishe kwa Mkoa wa Arusha hufanyika mara 2 kwa mwaka kwa lengo la kujadili hali halisi ya lishe kwa Mkoa na kubaini changamoto zilizojitokeza kwa kipindi hicho.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa