Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Serikali kusherehekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano kwa vitendo – kupitia ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuwafikishia wananchi huduma bora.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Aprili 25, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Akeri, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambapo ametembelea na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Wilaya hiyo.
“Rais Samia ameelekeza tuadhimishe miaka 61 ya Muungano wetu kwa kukagua miradi ya maendeleo. Wananchi hawahitaji maneno mengi, wanahitaji huduma na maendeleo — na hiyo ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Watanzania wanahitaji barabara bora, nishati ya kutosha, maji safi, huduma za afya na elimu bora, na Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kila sekta inaboreshwa kwa maslahi ya wananchi.
“Maendeleo yanahitaji hatua. Serikali ipo kazini kuleta huduma bora. Ni wajibu wetu kama wananchi kutaka kilicho bora kila wakati, na ni jukumu la Serikali kuhakikisha inakitekeleza,” ameongeza.
Aidha, Dkt. Biteko amewahimiza Watanzania kuuenzi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao umeendelea kuwa nguzo ya amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa