Na Elinipa Lupembe.
Imeelezwa kuwa, mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hasaan, yanatokana na maridhiano baina ya watanzania yanayoleta amani, utulivu na mshikamano na kuipa nafasi Serikali, kujikita kwenye kuleta maendeleo huku wananchi wakielekeza mawazo yao katika kufanya kazi za uzalishaji na kulijenga taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), na kusema kuwa, Serikali ya awamu ya sita, imefanya juhudi kubwa za kurejesha hali uzalendo unaobeba utaifa kwa watanzania wote, na kusababisha amani na utulivu nchini, mambo ambayo yalianza kupotea.
"Miradi mikubwa mnayoiona inayotekelezwa nchini, hususani kwenye mkoa wetu wa Arusha, katika sekta zote, tunashuhudia shule zinajengwa, barabara, miradi ya maji, na maendeleo ya kila aina, Utalii kupitia Serikali na sekta binafsi, yote ni matunda ya ushirikiano baina ya wananchi, viongozi na Serikali kwa pamoja wakiwa wanania mamoja" Amesema Mhe. Mongella
Amewaomba wananchi wa mkoa huo, kuendelea kudumisha ushirikiano miongoni mwao, kwa kuweka mbele utaifa na kujikita zaidi katika kufanya kazi ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa na kuwasihi viongozi wote wa jamii, dini, mila na Serikali kushirikiana katika shughuli zote za maendeleo na ujenzi wa Taifa.
Naye Katibu wa Chama cha ADP mkoa wa Arusha, Mussa Bayo, amempongeza mkuu wa mkoa wa Arusha, kwa kudumisha umoja na msikamano wa wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa kwa kuwa wanajenga nyumba moja.
"Nikupongeze mkuu wa mkoa, wewe ni kiongozi bora, umekuwa ukitualika kwenye vikao vya ushauri na sisi tunatoa ushauri kwa maendelo ya taifa letu na huu ndio mshikamano anaoutaka mama Samia, Wakuu wa wilaya igeni mfano " Ameweka wazi Katibu huyo wa ADP
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM , Mkoa wa Arusha, Loy Ole Sabaya, licha ya kupongeza viongozi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo amewasihi kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili thamani ya fedha zilizotolewa na serikali iweze kuonekana.
"Mradi ukikaa muda mrefu hata thamani ya fedha inashuka, bei ya vitu itabadilika na kusababisha ucheleweshwaji ambao unaondoa kabisa maana na malengo ya mradi husika, hivyo niwasihi wakurugenzi na wakuu wa Idara kusimamia miradi yote na ikamilike kwa wakati". Amesema Ole Sabaya.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Albano Mussa, amewasilisha hali ya uharibifu wa mazingira na miundombinu ya barabara unaotokana na ujenzi kwenye vyanzo vya maji na kingo za mito pamoja na uchimbaji wa moram kwenye vilima katika halmashauri za Arusha, Meru na Jiji la Arusha.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa