Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala, kuwasilisha Ofisini kwake orodha ya Taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na TEMESA ili aweze kuziandikia barua za kusisitiza kulipa madeni yao.
Agizo hilo amelitoa leo, mkoaninArusha wakati akifungua kongamano la Tatu la madereva wa Serikali, kwenye kituo cha mikutano ya Kimataifa Agosti 20, 2024 na kuwasisitiza Wakuu wa Taasisi wanaodaiwa na TEMESA kuhakikisha wanalipa madeni hayo mara moja ili TEMESA iweze kutekekeleza jukumu lake na kuhakikisha vyombo vya usafiri vinakuwa salama na vinatengenezwa kwa wakati.
“Wakuu wa Taasisi, popote mlipo mnanisikia, kama mpo hapa ndani au la, hakikisheni mnalipa madeni yenu TEMESA, mkiwalipa hawa matengenezo ya magari yenu yatafanyika kwa muda sahihi” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameipongeza TEMESA kwa kuwa na mitambo ya kisasa ya kutengeneza magari na kuwataka kuongeza ubunifu na uadilifu ili kuleta tija katika utengenezaji wa magari ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi kuthamini kada ya madereva kwa kuwapa mahitaji yao ili wafanye kazi kwa ufanisi na hivyo kulinda usalama wa viongozi, wananchi na magari wanayoyaendesha.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini mchango wa madereva nchini na itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto za madereva ili kuikuza kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Naye Naibu waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kukilea chama cha madereva ili kikue na kufanya kazi kwa weledi.
"Wizara itahakikisha madereva wanapata elimu stahiki ya magari wanayoyaendesha ili kuendelea na ukuaji wa teknolojia na kuwawezesha kushiriki vikao vyao ili kukuza weledi.
Jumla ya adereva 1,300 kutoka Tanzania bara na Zanzibar wanashiriki kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo " Dereva wa Serikali jitambue, timiza wajibu wako, usalama barabarani unaanza na wewe kazi iendelee".
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa