Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia amewataka wamiliki wote wa vituo vya kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wanapata leseni za kutolea huduma hiyo ifikapo Desemba 2021.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau na wamiliki wa vituo vya kulele watoto waishio katika mazingira magumu,Jijini Arusha.
Leseni itawasaidia kufanya kazi kwa uhakika na kwa kufuata sheria na taratibu.
Mkoa wa Arusha unajumla ya makao 89 ya watoto waishio katika mazingira magumu na amesema si jambo la kujivunia kwa kuwa na makao mengi ya watoto na hii inaonesha ni kushindwa kwa wazazi kuwajibika ipasavyo.
Kati ya makao hayo ni 36 tu ndio yanafanya vizuri na wapo wanaofanya kazi hiyo kwa wastani na wengine hawaelewi taratibu za kufuata katika kuwahudumia watoto.
Amewataka hao wasio elewa taratibu wajitadhimini kwani suala hilo lipo kisheria hivyo zifuatwe.
Aidha, Dkt. Kihamia ametoa maelekezo ya kufuatwa na wamiliki wa makazi hayo ya watoto, akiwemo kuwapatia bima ya Afya iliyoboreshwa watoto wote ili kupunguza gharama za matibabu.
Pia, huduma zinazotolewa kwenye vituo hivyo ziwe za kiwango kinachotakiwa, Maafisa ustawi wa Jamii na Maafisa Afya wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo hivyo.
Makao hayo yawe na wataalamu wanaojua kanuni na sheria za makao hayo ili waweze kuzitekeleza kwa urahisi.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kutoa mrejesho wa namna wadau hao wa makao ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wanavyotoa huduma.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa