Na Elinipa Lupembe.
Kufuatia mkakati wa kupambana na mila na desturi potofu zinazosababisha ndoa za utotoni kwa wasichana wa jamii ya kimaasai, Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3 za kujenga shule ya sekondari ya wasichana wilaya ya Longido.
Shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule zinazojengwa nchini, mkoa wa Arusha umepata fedha za ujenzi wa shule hiyo maalum kwa wasichan, shule ambayo inakwenda kutatua changamoto ya wasichana waloikuwa wakikosa fursa ya kusoma kutokana na mila na desturi za jamii ya wafugaji.
Akizungumza wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella, ameweka wazi kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya kwenda shule huku kukiwa na msisitizo kwa wasichana wa jamii ya wafugaji, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa elimu kutokana na kuozeshwa katika umri mdogo.
Amesema kuwa, Serikali ya Mama Samia, imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu, ambapo jamii kubwa ya wasichana wa kimaasai, nayo imepewa kiapumbele, kupitia ujenzi wa shule hiyo inayotarajiwa kuwa na michepuo ya masomo yote ikiwa ni shule ya bweni.
"Tunamshukuru Mheshiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaangalia wasichana wa jamii ya Kimasaai kwa jicho la kipekee, ujenzi wa shule hii, utaleta mapinduzi makubwa ya kielimu na kijamii kwa wafugaji". Amesema Mhe. Mongella
Hata hivyo, wananchi wa Jamii ya wafugaji, hawakusita kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali na kuwajengea shule kubwa, nzuri na ya kisasa, maalum kwa watoto wao wa kike, jambo ambalo wamekiri, hiyo ni neema ya Mungu kwa kuwa, hawakuwahi kuwa na ndoto hiyo.
Mjumbe wa kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Salome Melubo Laizer, amesema kuwa, kutokana na kampeni nyingi za kumkomboa msichana wa jamii ya kimaasai, Serikali imekuja na tiba ya ugonjwa sugu ambao, hata walipotaka kumtibu msichana walikosa wodi ya kumlaza, kwa sasa watoto wao wamepata kimbilio sahihi na salama, watalala shuleni.
"Shule hii ni tiba kwa wasichana wetu, sasa watasoma kama watoto wengine wa kitanzania, kinamama tulitamani wasichana wetu wasome, lakini hatukuwa na mahali pa kuwapeleka, kutokana na mila za kabila letu wengi waliishia kuolewa badala ya kusoma" Amekiri Neema Lasirasi
Mayoni Laiza, amethibitisha umuhimu wa shule hiyo, kwa jamio ya wafugaji, kutokana na kuwa karibu karibu na eneo hili, lakini zaidi shule hiyo ni kubwa ambayo itachukua wanafunzi wengi, ambao awali walikosa nafasi ya masomo kutokana na kutokuwepo na shule karibu.
AwalI, Kaimu Mkuu, wa Idara ya Ujenzi, Hlamashauri ya Longido Mhandishi Grace Siriaki, amefafanua kuwa, shilingi Bilioni 3 zinatumika kujenga, jengo la utawala, vyumba 12 vya madarasa, mabweni 8, nyumba mbili za walimu, ukumni wa mikutano na bwalo la chakula.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa