@ortamisemi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wakuu wa mikoa na watendaji wengine wa mamlaka za serikali za mitaa nchini kuhakikisha wanaongeza kasi ya usikilizaji kero za wananchi na kuzitatua.
Mhe. Mchengerwa amewatska watendaji hao kutomsubiri Rais Dk. Samia Suluhu Hassan afanye hivyo kwakuwa wamepewa mamlaka makubwa ya kusimamia maeneo yao.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo jijini hapa wakati akizindua Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa gharama ya sh. bilioni 400 ambao utagharamiwa na serikali pamoja na washirika wa maendeleo.
Mhe. Mchengerwa amesema dhamira ya programu hiyo ni kuamsha chachu ya utendaji kazi katika maeneo yao ya utawala huku akieleza kuwa kazi kubwa imeshafanyika.
“Leo hii tukimsimamisha kila mkuu wa mkoa hapa ataeleza mabilioni yaliyoingia katika mkoa wake, hatuna sababu yoyote ya kurudi nyuma kwa kazi kubwa ambayo Dk. Samia amefanya.
Rais ametuletea programu hii ili tuboreshe maeneo ya utendaji kazi wetu, kazi tuliyobaki nayo ni utoaji wa huduma, kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.”
Aliongeza kuwa “Ninakiri kazi kubwa ambayo wakuu wa mikoa mnafanya, nilipoingia na sasa tofauti ni kubwa sana watendaji wanafanya kazi, umoja na mshikamano umeimarika.”
“Rais anawaona mnapoenda site na kusikiliza kero za wananchi anawaona, kazi tuliyonayo sasa ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, Rais amenituma niseme hii, sasa hivi watu hawakai maofisini kama ilivyokuwa zamani, ule U-mungu mtu umekwisha. tuendelee kujishusha kuwa wanyeyekevu kwa watanzania kwa sababu ndio wenye nchi yao.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa