Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 2,244 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika, sasa Tanzania Bara.
Kati ya wafungwa hao, 263 wataachiliwa huru leo Desemba 9, 2023 huku wafungwa wawili waliokuwa na adhabu ya kifo wakibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha misha jela.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, wafungwa wengine 1,979 wamepunguziwa sehemu ya adhabu zao ambazo wataendelea kuzitumikia gerezani.
“Ni matumaini ya Serikali kwamba wafungwa walioachiliwa huru leo Desemba 9, 2023 watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais ametoa msahama huo kupitia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa kwa kufuata masharti.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa