Mbele ya wanahabari Jijini Arusha leo Jumatatu Septemba 23, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema takribani nchi 9 kutoka Barani Afrika zimethibitisha kushiriki kwenye Land rover Festival 2024 inayotarajiwa kufanyika Oktoba 12-14 mwaka huu.
Mhe. Makonda amesema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 na kuendelea kutoa wito kwa wanafamilia ya Land Rover kuendelea kujisajili kwa wingi ili kuweza kuvunja rekodi iliyokuwa imeweka na Ujerumani kwa kuwa na msafara mkubwa zaidi wa magari aina ya Land Rover.
"Tuna ndoto kama Taifa ya kuvunja rekodi ya Guiness iliyoandikwa na Ujerumani kwa kuwa na magari 632, sisi mkoa wa Arusha tunataka kuwa na magari 1000. Kwa lugha nyepesi ni kwamba unapojisajili sio kwasababu tunataka tukutambue tu, tunataka tuvunje rekodi. Naomba tuendelee kujisajili ili uwe sehemu ya wavunja rekodi walioandika historia kwa kuwa na parade refu kuliko parade zote duniani za magari ya kampuni aina ya Land Rover." Amesema Mhe. Makonda.
Kulingana na maelezo ya Mhe. Makonda, Parade hiyo ya Matoleo yote ya Land Rover litakuwa na Urefu wa Kilomita zaidi ya 12 na washiriki wa Land Rover Festival 2024 watapata fursa pia ya kutalii bure kwenye hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa kutumia magari yao huku pia kukitengwa maeneo mbalimbali ya kuburudika pamoja na maeneo kwaajili ya michezo ya watoto.
_Kwa kujisajili na kwa maelezo zaidi wasiliana na waandaaji wa Land Rover Festival 2024 kupitia tovuti ya "landroverfestival.co.tz" au kwa simu namba +255682725555
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa