Mkoa wa Arusha unategemea kupokea Mwenge wa Uhuru 2024, siku ya Ijumaa tarehe 19 Julai, 2024,kwenye viwanja vya shule ya Msingi Migungani, Kijiji cha Migungani, Kata ya Mbuguni wilaya ya Arumeru, ukitokea Mkoa wa Manyara.
Ukiwa mkoani Arusha, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Godfrey Eliakimu Mnzava atakimbiza Mwenge huo wa Uhuru umbali wa Kilomita 1,189.35 , kwenye wilaya sita na halmashauri zote saba za mkoa wa Arusha, na kupitia jumla miradi 65 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 61. 6.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ataweka mawe ya msingi miradi 18, atafungua mradi 1, atazindua miradi 12 na kutembelea miradi 34 ya katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Miundombinu ya Barabara, Uwezeshaji vijana Kiuchumi, Biashara na Ujasiriamali, Lishe, Klabu za Vijana wapinga Rushwa, Makundi Maalum, Uhifadhi wa Mazingira pamoja na kutoa salamu na ujumbe wa Mwenge wa Uhuru katika halmashauri zote.
Aidha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru atatembelea Miradi ya Maendeleo iliyowekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka uliopita wa 2023.
Aidha, Mwenge wa Uhuru 2024, unaadhimisha kumbukizi ya 60 tatu, ikiwa ni pamoja na kuadhimisha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ukihamasisha watanzania wote kuimarisha na kudumisha Umoja na mshikamano kwa kuweka mbele uzalendo na kuilinda tunu ya amani ya nchi ya Tanzania.
Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ni "Tunza Mazingira, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu", ukiwa na Jumbe za Kudumu za Mwenge wa Uhuru za Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malari, matumizi ya Dawa za Kulevya, VVU - UKIMWI na Rushwa sambamba na kuhamasisha wananchi kuzingatia Lishe Bora pamoja na kujiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa