NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA NDUGU MOGELLA AKABIDHI OFISI NA KUWAAGA WANAARUSHA
Na Elinipa Lupembe
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Arusha na kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu Chama cha Mapinduzi Tanzania Bara, Ndugu John V.K Mongella, amepata wasaa wa kuagana na wananchi wa Mkoa wa Arusha, muda mfupi baada ya kumkabidhi Ofisi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa huo mapema leo Aprili 8, 2024.
Ndugu, Mongella licha ya kuanza kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu, amewashukuru wananchi wote wa Arusha, kwa ushirikiano mkubwa waliompa kwa kipindi cha miaka mitatu, alichotumika kama Mkuu wa Mkoa, na kuwasisitiza viongozi, wadau na wananchi wote, kumpa ushirikiano Mkuu wa Mkoa mpya Mhe. Makonda.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo, amekiri kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wote wa Mila, Dini, Chama na Serikali ambao kwa pamoja ndio wadau wakubwa wa Maendeleo ya Mkoa, huku akijivunia kuwa, Mkoa wa Arusha umefanyika baraka katika maisha yake, eneo ambalo alipata uteuzi kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa na hatimaye kwa mara nyingine kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara, akiwa Arusha.
"Niwaombe wanaarusha kumpa ushirikiano Mhe. Makonda, ninamuamini kuwa ni kiongozi jasiri na mwenye uzoefu, mwenye kasi ya maendeleo, tuendelee kushikamana kwa mustakabali wa Mkoa wetu wa Arusha na Taifa, Mhe. Makonda ni mchapakazi anayetaka matokeo ya haraka" Amesema Mongella.
Aidha, amekiri kuwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Arusha ni watu mahiri, wazalendo, wenye uchu wa maendeleo, wenye uchungu na Mkoa wao na Taifa lao la Tanzania, ambao walimsukuma kufanya kazi wakati wote.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, pamoja na kwenda eneo jingine la kazi, yeye ni mdau wa Arusha, mafanikio ya Arusha yatamgusa moja kwa moja, na yuko tayari kutoa ushauri pamoja na kuchangia, maendeleo ya Arusha pale itakapohitajika.
Awali, Ndugu Mongella amemkabidhi rasmi Ofisi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, ikiwa ni pamoja na zana za kufanyia kazi ikiwemo taarifa ya Maendeleo ya Mkoa wa Arusha.
#ArushaFursaLukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa