Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Geophrey Pinda (mb) amekabidhi jumla ya Hatimiliki za ardhi 240 kwa wananchi walionunua viwanja kutoka Shirika la Nyumba la Taifa NHC mkoani Arusha.
Mhe. Pinda amewataka wananchi wa Arusha kutambua thamani ya hati hizi ikiwa ni pamoja na kuzilinda kwani zina faida kubwa hasa fursa ya kukopa fedha kutoka taasisi za kifedha kama benki .
"Hati thamani yake ni kubwa sana kwenye Maisha yetu ya leo , niwaombe maana hii hata kama ungetaka kujenga ghorofa kumi hii tu peke yake ni neno kwa wenye mapesa yao ukienda benki utazaminiwa na leo tunatoa kama hati 240″.Amesema Pinda.
Aidha Pinda amewasihi watumishi wa Ardhi kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia lugha nzuri na kuacha kuzua taharuki kwa wananchi katika kufuatilia huduma za kiardhi katika ofisi zao
“Mtumishi ukibainika umeshiriki kwenye tatizo linalosababisha mwananchi asioate hati yake kwa wakati hatukuhamishi inawezekana Umechoka kufanya kazi Wizara ya ardhi”amesema.
Aidha Pinda amemtaka Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Jijini Arusha kuacha kuuza nyumba zilizopo mjini humo badala yake nyumba hizo zote zilizopo katikati ya miji zisiuzwe badala yake yajengwe majengo yenye uhitaji na maeneo ya mjini.
“Vijumba vingine vilivyopo katikati miji kwa kweli vya NHC ni vya urithi havina sura ya Tanzania ya Sasa hivi vibomelewe muende mkazijenge upya ili tupate thamani inayofanana na uhalisii” amesema Pinda.
Kwa upande wake Meneja wa shirika la nyumba kanda ya kaskazini ,Benit Masika .akisoma ripoti ya mradi wa Safari City amesema kuwa mradi huu upo eneo la Burka Mateves ndani ya Jiji la Arusha ambapo umeandaliwa katika eneo la ekari 587 katika mpango kabambe uliondaliwa mwaka 2014.
Amesema kuwa ,mradi huu una jumla ya na viwanja 1913 kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba za makazi, majengo ya biashara, huduma za jamii kama shule, vyuo, hospitali, sehemu za kiibada, sehemu za michezo, sehemu za mapumziko na maeneo ya usalama wa mji kama kituo cha polisi na zimamoto na maeneo ya viwanda vidogo vidogo ambapo pia kuna maeneo ya wazi.
“Katika viwanja hivyo 1913, Shirika limetenga viwanja 1601 kwa ajili ya kuviuza sawa na asilimia 84%, na viwanja 313 Shirika limevihifadhi (retained) sawa na asilimia 16% kwaajili ya uendelezaji wa baadaye.
Amefafanua kuwa,kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Juni, 2016 hadi sasa Shirika la Nyumba limeweza kuuza jumla ya viwanja 1026 sawa na asilimia 63.8% ya jumla ya viwanja vyote vilivyotengwa kwa ajili ya mauzo vyenye thamani ya sh. 21,024,916,000 ambapo mpaka sasa Shirika limekusanya kiasi cha sh.12,955,300,290 sawa na asilimia sitini na moja (61%) ya mauzo ambapo kiasi kilichobakia cha sh.8,069,615,710.
Shirika linaendelea na utaratibu wa kufuatilia ulipaji wa pesa hiyo kwa wateja wetu, ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha wateja kulipia (kupitia demand notices) kama inavyotakiwa kwenye utaratibu wa malipo yaani payment plan ya kila mteja ili kuhakikisha kila mteja anatimiza wajibu wake wa kulipia kiwanja ndani ya muda husika aliopewa.
Aidha kati ya viwanja 1026 vilivyouzwa, jumla ya viwanja 350 tayari wateja wameshamaliza malipo ya viwanja hivyo kwa asilimia 100. Idadi hii ni sawa na asilimia 34% ya wanunuzi wote ambapo wateja 295 tayari wamekabidhiwa hati miliki zao.
Aidha amefafanua kuwa , katika viwanja vilivyobakia kwa ajili ya kuviuza, ambavyo ni jumla ya viwanja 579, kutokana na mabadiliko ya kijeografia na kimazingira ya eneo hili la SafariCity, jumla ya viwanja 540 vipo kwenye mpango wa kufanyiwa marekebisho ya upimaji ili viweze kukidhi mahitaji ya watanzania wanaotaka kuwekeza katika mradi huu.
Bei ya kiwanja ni Sh.21,000 kwa mita ya moja mraba kwa maeneo ya makazi na sh.27,000 kwa mita moja ya mraba kwa maeneo ya biashara, ambapo mteja anapatiwa fursa ya kulipia kidogokidogo kwa muda wa miezi 36 kwa upande wa viwanja vya makazi, na kwa upande wa viwanja vya biashara, mteja anaweza kulipia kidogo kidogo ndani ya muda wa miezi 60 yaani miaka mitano, ambapo kila mwezi mteja anaweza kulipia kiasi cha sh. 131,000/= tu bila riba yoyote.
“Kuhusu uendelezaji wa viwanja, ieleweke kwamba Shirika la Nyumba liliazimia kuuza viwanja katika mradi huu wa SafariCity kwa malengo ya kutoa fursa ya uendelezaji kwa wadau yaani wanunuzi na mpaka sasa kuna jumla ya wanunuzi 25 wanaendelea na ujenzi wa viwanja vyao huku wanunuzi 4 kati ya hao tayari wamekwishahamia kwenye makazi yao.”amesema.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa