Rais Samia Suluhu Hassan amewaasa wananchi kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa ili iendelee kudumu na kuimarisha uchumi wa nchi za Afrika Mashariki ( EAC).
Aidha, amemhakikishia Rais Uhuru Kenyatta ambaye anamaliza muda wake wa uongozi hivi karibuni mipango yote waliojiwekea ikiwemo ujenzi na miundo mbinu ya barabara ataikamilisha kama walivyokubaliana kwenye vikao vyao.
Akizungumza hayo jijini Arusha wakati alipokuwa kwenye hafla ya ufunguzi wa barabara ya Arusha Bypass ya Km.42.4 yenye thamani ya Dola milioni 217 kutoka Benki ya Maendelo ya Afrika (AfDB) ambayo kwa Tanzania imetumika Dola milioni 212 na Kenya milioni 105.
Alisema ameona licha ya jitihada za ujenzi wa miundombinu unaofanywa na serikali pamoja na nchi za EAC kumezuka tabia ya uharibifu wa miundo mbinu hiyo ikiwemo kuiba vyuma vya madaraja na utupaji wa taka kwenye madaraja.
"Niwaombe sana watanzania tuheshimu na kufuata taratibu zilizowekwa katika utunzaji wa barabara kwa sababu imezuka tabia ya baadhi ya watu kuharibu miundo ya barabara pamoja na kutengeneza magari barabarani na kumwaga mafuta machafu yanayosababisha kuharibu miundombinu ya barabara iliyotengenezwa kwa fedha nyingi,"alisema.
Samia,alisema serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ya Reli,barabara,usafiri wa anga na majini ili kuunganisha nchi za EAC.
Aidha aliwataka wananchi ambao miundombinu hiyo inatekelezeka katika maeneo yao kutumia fursa za ujenzi wa miundombinu hiyo kujikwamua kiuchumi.
Rais Uhuru Kenyatta aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono viongozi wa nchi za EAC ili waendelee kuashirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo kupitia umoja wao ambao utasababisha waheshimike na mataifa makubwa Dunia.
" Ni ishara kubwa kuwa viongozi tukiungwa mkono tukashirikiana kwa pamoja hakuna changamoto itakayotushinda tutafanya maendeleo makubwa kupitia umoja wetu na kuheshimika na mataifa Makubwa Duniani,"alisema .
Kuhusu barabara hiyo Rais Kenyatta alisema itasaidia kuunganisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kurahisisha usafiri wa bidhaa mbalimbali za mboga mboga na mazao ya biashara.
"Huu ni utajiri mkubwa wa fursa katika kukuza uchumi wa nchi wanachama hasa kwa wakulima wa Tanzania ambao gharama za kusafirisha mazao yao zitapungua kutokana na uwepo wa barabara hii,"alisema
Kenyatta alitumia fursa hiyo kumpomgeza Rais Samia ambaye alipokea nchi katika kipindi cha majonzi na watu wengi walikua na hofu,lakini amekuwaa hodari na mchapakazi na Taifa linasonga mbele.
"Kuna msemo wa Kiswahili unasema, usimuone Simba amenyeshewa ukadhani ni Paka dada yangu Rais Samia alipokea nchi katika kipindi cha majonzi na wengi walikuwa na hofu,lakini amekuwa ujasiri na mchapa kazi,"alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Dk.Peter Mathuki alisema Afrika inahitaji kufikia mtengamano katika kukuza uchumi kwa kuwa na Miundombinu imara na viwanda vya kutengeneza bidhaa zitakazokuza uchumi.
"Barabara hii ni muhimu katika kuimarisha biashara kwa nchi wanachama wa EAC", alisema.
Alisema moja ya mipango ya EAC ni kuimarisha uchumi ambapo wameweka vipaumbele vitano vilivyopewa msukumo mkubwa.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni usafiri wa anga,Reli,Tehama,bandari na usafiri wa majini.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa alisema barabara hiyo itapunguza urefu wa safari kutoka Tanzania hadi Mombasa nchini Kenya.
Alisema barabara hiyo itafungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii kwa nchi wanachama hasa Tanzania.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania Patricia Laverley benki hiyo imetoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia maendeleo na kuimarisha uchumi kwa nchi za EAC.
Aliahidi kuendelea kushirikiana na nchi za EAC katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu wamekiri malengo ya kuanzishwa kwa benki hiyo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa