Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewataka wakufunzi wa sensa kuwa wazalendo, waadilifu na kufanya kazi kwa weredi katika zoezi la kutoa mafunzo ya sensa.
Ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya wakufunzi wa sensa kwa Mkoa wa Arusha yaliyofanyika Jijini Arusha.
Zoezi la sensa ni muhimu kwani litasaidia kupata taarifa ya msingi kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, Mhe.Mongella amesisitiza kuwa mipango makini inaendana na idadi ya watu.
Pia, zoezi hili litaenda kutengeneza msingi na mstakabali wa maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha bwana Zelothe Steven, amewahasa wakufunzi hao kuwa wamebeba dhamana ya Mkoa hivyo wakaufanye Mkoa kuwa kinara.
Nae, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha bwana Said Mabie amesema changamoto kubwa ya watu wa mipango ni kutokuwa na data safi zitakazowasaidia kuweka mipango sahihi kulingana na mahitaji.
Hivyo kupitia sensa ya mwaka huu idara ya mipango itaweza kuweka mipango inayotekelezeka zaidi.
Akielezea hali ya mafunzo hayo Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo bwana Mdoka Omary amesema kwa Mkoa wa Arusha jumla ya wakufunzi 399 wamepatiwa mafunzo ya sensa kwa ajili ya kufundisha makalani wa sensa katika kila halmashauri.
Amesema pia, mafunzo hayo yamefanyika takribani kwa wiki 3 ikijumuisha watumishi kutoka ngazi ya halmshauri na Mkoa, watu wenye ulemavu na taasisi binafsi za Mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa