Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema ongezeko la asilimia 35.1 la kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma lililotangazwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni ishara ya wazi ya dhamira ya Serikali kuboresha maslahi ya watumishi na kuwataka watumishi kuongeza tija na uadilifu katika kazi zao.
Akizungumza Mei 2, 2025 na watumishi wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa Wizara yake inasimamia zaidi ya asilimia 76 ya watumishi wote serikalini, hivyo ni muhimu kwao kuonyesha uzalendo kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kusaidia katika kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, ameeleza kuwa hatua ya Rais Samia imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizotoa ongezeko kubwa la mishahara kwa watumishi wake, akisisitiza kuwa hiyo ni fursa adimu inayopaswa kutumiwa kwa kuwajibika kikamilifu.
Hata hivyo, amewataka wataalamu wa serikali katika Halmashauri zote kutumia mabaraza ya madiwani kuendeleza mijadala ya maendeleo badala ya siasa zisizo na tija, huku akiwaonya watumishi wasio waaminifu kubadilika kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, kwa ubunifu katika kusimamia maendeleo, Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa viongozi wa mikoa na halmashauri wanapaswa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato huku wakidhibiti mianya ya upotevu ili kujenga taifa imara lisilo tegemezi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa