Mkuu wa Mkoa wa Arusha amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa sanaa, utamaduni na michezo Prof. Palamagamba Kabudi, ambaye yupo mkoani Arusha kukagua maendeleo ya Ujenzi wa uwanja wa michezo unaojengwa Mkoani Arusha kwaajili ya mashindano ya Kandanda kwa mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON 2027.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Kabudi amempongeza Mhe. Makonda kwa mashindano na matukio mbalimbali ya kimichezo aliyoyaratibu na kuyasimamia, ikiwemo Land Rover Festival 2024, ambayo imesaidia kuitangaza Arusha kimataifa na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha waliouza bidhaa na huduma mbalimbali wakati wa tamasha hilo pamoja na mashindano mengine ya kimichezo yaliyofanyika Jijini Arusha tangu kuteuliwa kwake.
Kwa upande wake Mhe. Makonda ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha unazidi kufunguka kitalii ambapo kwasasa Utalii wa safari na michezo ndiyo ajenda kuu ya Mkoa na Rais Samia pia anaendelea na mpango wake wa kutambulisha utalii wa matibabu katika Mkoa huo kando ya utalii wa kitamaduni ambao Mkoa wa Arusha utaanzisha maonesho yake kuanzia mwezi Machi mwaka huu, kwa kukutanisha jamii mbalimbali za kigeni zilizopo mkoani hapa kwaajili ya kuonesha tamaduni zao mbalimbali.
Mashindano ya AFCON 2027 yatafanyika kwa ushirikiano wa wenyeji wa nchi tatu, Tanzania, Kenya na Uganda ambapo kwa Tanzania viwanja kadhaa vitatumika katika michuano hiyo ikiwemo uwanja mpya unaojengwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, eneo la Bondeni city Jijini Arusha, serikali pia ikitarajia kujenga mji wa biashara pembezoni mwa uwanja huo ili kutoa fursa kwa wakazi wa Arusha kunufaika kiuchumi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa