Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua kikao kazi cha Wenyeviti wa bodi na Watendaji wakuu wa Taasisi za serikali (CEO FORUM 2024), Mkutano utakaofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha kwenye kituo cha kimataifa cha Mikutano cha AICC.
Mkutano huo wa siku nne, umeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina una lengo la kuwahamasisha na kuwashirikisha watendaji hao wa Taasisi, Mashirika na Wakala za Serikali kuhusu Maboresho yanayoendelea katika kuimarisha usimamizi, uendeshaji na utendaji wa Taasisi za umma sambamba na kubadilisha uzoefu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewaambia wanahabari kuwa kikao hicho kitafunguliwa rasmi Agosti 28, 2024, siku moja baada ya watendaji hao kuanza kukutana na kikitarajiwa kufungwa rasmi Agosti 30 ya mwaka huu.
"Ugeni huu mzito wa Dkt. Samia Suluhu Hassan unakuja na fursa lukuki na kwakweli ni hakika amani na utulivu wa mkoa wetu, Upendo na mshikamano na shughuli za kiuchumi zinazoendelea zinachagizwa na kazi kubwa njema anayoifanya Dkt. Samia ya kuhamasisha utalii, na sasa anasukuma gurudumu la kuhakikisha Arusha inakuwa kitovu cha mikutano ya Kimataifa tukianza na mikutano ya ndani." Ameongeza kusema.
Mhe. Makonda ametumia fursa pia kuwaomba wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwataka pia kutumia ugeni huo kuweza kujinufaisha kupitia fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa