Na Prisca Libaga.
RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutotegemea wahisani kutoka ughaibuni kama misaada ya kupambana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya hewa
Alisema bara la Afrika ni mama wa mazingira hivyo nchi za EAC zisikubali tena kuharibu mazingira kwa kutegemea misaada ya kifedha kutoka nchi.
RAIS alisema hayo jana kwenye Mkutano wa ngazi ya juu wa 23 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha wakati akiwahutubia viongozi mbalimbali wakiwemo marais watatu na wawakilishi wa marais 3 wa EAC
"Tusiwategemee wengine kuja kutupa fedha za majanga ya mabadiliko ya hali ya hewa.Nashauri huu uwe ujumbe wetu kwa nchi za EAC kwenye mkutano ujao wa dunia wa COP28 kuhusu mazingira" alisema
Alisema bara la Afrika bado lina mazingira mazuri sana na kuna fursa hivyo mataifa ya nje wanapenda kuja kutumia rasilimali hivyo nchi za EAC zinatakiwa kuanza kutumia mapato yake kwenye majanga ya tabianchi
"Wenzetu huko wameishaharibu hawana mazingira tena. Tunatakiwa kulinda mazingira yetu, hivyo tukatae masharti. Haiwezekani sisi tunalinda halafu makampuni ya nje yanakuja kuvuna" alisema
Rais pia alizitaja juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kukabiliana na majanga ya mabadiliko ya tabia nchi
Baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na serikali kuondoa kodi kwenye pembejeo za kilimo kwa ajili ya kukuza kilimo na usalama wa chakula, kuondoa ushuru na vivutio vyote vya kodi kwenye bidhaa zinazotumika kuzalisha nishati mbadala kwa ajili ya kulinda mazingira.
"Sasa hivi tunahamasisha sekta binafsi kuchangamkia fursa zinazotokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuanzisha vituo vya utafiti nchi nzima. Hapa tunataka sekta binafsi washiriki kwa kuongeza thamani bidhaa za mazao ya kilimo" alisema
Kwa Upande wake Mwenyekiti anayemaliza muda wa EAC RAIS wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye alisema dunia iko kwenye matatizo makubwa ya ukame na mafuriko hivyo nchi za EAC lazima zinatakiwa kwa pamoja kuja upya na sera mpya zitakazozinusuru kutoka kwenye janga la mabadiliko ya tabia nchi.
"Tunahitaji kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dni na wadau wengine wa maendeleo" alisema
Alisema mahitaji makubwa kwa nchi za EAC ni kuwa na teknolojia, uafiti wa kina na uwekezaji katika masuala ya mazingira
"Ili kuwa na usalama wa chakula lazima tuwekeze kwenye utafiti na teknolojia na tunahitaji sera ya kanda kuhusu mabadiliko ya tabia nchi" alisema
Mkutano wa Wakuu wa Nchi unahirishwa jana kwa Rais wa Ndayishimiye kukabidhi kijiti kwa Rais Salva Kiir wa Jamhuri ya Sudan Kusini. Katika mkutano huu Marais Paul Kagame (Rwanda), Felix Tshekedi ((DR Congo) wametuma wawakilishi
Mwisho
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa