Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumanne Septemba 02, 2025 akiwa ziarani Wilayani Ngorongoro, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuwa watulivu na kuendelea kudumisha amani na Mshikamano miongoni mwao, wakati wakisubiri majibu ya Tume mbili zilizoundwa na na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sale Kata ya Sale kwenye Mkutano wa hadhara, Mhe. Makalla amebainisha kuwa kwa Busara, hekima na mapenzi ya Rais Samia kwa wananchi wa Ngorongoro, tayari Tume hizo zimekabidhi ripoti kwa Rais Samia na punde baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, hatma na maamuzi ya serikali yatatangazwa hadharani.
"Niwaombe, tumesubiri muda wa kutosha, tumeipa tume muda wa kutosha, hatuwezi kushindwa kusubiri muda mdogo uliobaki tukapata majibu. Niwaombe Wazee na Viongozi wa mila wa Ngorongoro, tumahitaji hekima zenu, uongozi wenu utukubalie tumpe nafasi Mhe. Rais amalize uchaguzi na hili la kutangaza matokeo ya taarifa za Tume itakuwa moja ya kipaumbele cha mapema baada ya uchaguzi." Amesema Mhe. Makalla.
Akisisitiza kuwa kuundwa kwa tume hizo mbili kulitokana na hekima na busara ya Rais Samia kutaka kupata mawazo na ushauri kwa mawanda mapana zaidi, Mhe. Makalla pia amewataka wananchi kujiepusha na wanasiasa na baadhi ya wananchi wanaowashinikiza kutosubiri matokeo ya Tume hizo, akisema Rais Samia ana dhamira njema na mapenzi makubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro.
Rais Samia wakati alipokutana na Viongozi wa Jamii ya Kimasai Mkoani Arusha alitangaza kuunda timu mbili, Moja ikihusika na tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na ya pili ilipewa kazi ya kuangalia utekelezaji wa uhamaji wa hiari kutoka eneo la hifadhi kwenda Msomera, Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa