__Ameahidi kushughulikia upatikanaji wa Skana kituoni hapo__
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla @amosmakalla leo Alhamisi Septemba 04, 2025 ametembelea na kukagua utoaji wa huduma kwenye Kituo cha forodha cha Pamoja kwenye Mpaka wa Namanga Mkoani Arusha, akiwataka watumishi wa Taasisi zote 18 za serikali zinazotoa huduma kwenye kituo hicho kuongeza ufanisi katika utendaji ili kukuza biashara kati ya Mataifa ya Tanzania na Kenya.
Aidha Mhe. Makalla akizungumza na Watumishi wa Taasisi hizo ameahidi kushirikiana na Waziri wa fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba @mwigulunchemba na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda @tratanzania kuhakikisha inapatikana Skana ya ukaguzi wa mizigo kwenye kituo hicho cha forodha ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wageni na watanzania wanaotumia mpaka huo kuingia nchini.
"Skana kwa Tanzania ipatikane haraka, haiwezekani kwa mapato haya tukose Skana, tupate skana turahisishe biashara na ile adhma ya kurahisisha biashara tuione kwa vitendo ili sisi tusiwe kikwazo, nitalisukuma hili kwa nguvu zote na skana tuipate kwa uharaka." Amesema Mhe. Makalla wakati akizungumza na watumishi kutoka Taasisi 18 za serikali zinazofanya kazi kwenye kituo cha Namanga.
Katika maelezo yake, Mhe. Makalla pia amewakumbusha watumishi hao kuwa wamebeba dhamana na taswira ya nchi katika kutoa huduma kwa wageni na watalii wanaoingia nchini kwa kupitia mpaka wa Namanga akiwahimiza pia kufanya kazi kwa bidii katika kutimiza malengo na maono ya Viongozi wa pande mbili, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan @samia_suluhu_hassan na Rais Dkt. William Ruto wa Kenya.
Awali wakati akimkaribisha kwenye Kituo hicho cha Namanga, Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Salum Kalli amemueleza Mhe. Makalla kuwa kupatikana kwa Skana hiyo kutarahisisha zaidi biashara na muingiliano wa watu kupitia mpaka huo pamoja na kupunguza muda mrefu unaotumika kwenye ukaguzi wa magari ya mizigo yanayoingia nchini kupitia mpaka huo unaotumika kwenda Kenya, Uganda, Sudani Kusini na Somalia.
@maelezonews @urtmof @tratanzania @ppra_tanzania @monduli_dc @longido.di
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa