Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameagiza watoa huduma za msaada wa kisheria kwenye kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia, kuhakikisha kuwa wananchi wote waliofika kupata msaada wa kisheria wanasikilizwa na kutatuliwa changamoto zao kikamilifu.
Rc Makonda ameyasema hayo leo Machi 01, 2025 wakati akizungumza na wananchi mbalimbali waliofika katika Banda la Wizara ya Katiba na Sheria kupata msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Samia Legal Aid Campaign inayotolewa viwanja vya TBA, ikiwa ni siku ya kwanza ya zoezi hilo Mkoani Arusha.
Mhe. Makonda amesema wananchi wanaofika katika banda hilo wanatakiwa kusikilizwa na kuhudumiwa ili waweze kutoa malalamiko yao ikiwemo kuangalia kwa makini changamoto zao hususani katika idara ya kazi, sheria, haki za watoto na mengineyo.
Mhe. Makonda ametumia fursa hiyo pia kuwasihi wananchi wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupatiwa msaada huo wa kisheria ili migogoro yao iweze kutatuliwa kupitia uwezeshaji uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan uliotokana na wazo lake hili la kuwa na kampeni ya kitaifa ili kuwafikia wananchi wanyonge na wale wanaokosa haki zao kulingana na sheria.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa