Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Ijumaa Machi 28, 2025, amewataka Wanasheria na Mawakili wanaotekeleza kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Arusha kuipatia ofisi yake majina ya watendaji na Viongozi wanaotajwa na wananchi kuwa vyanzo na wachochezi wa migogoro ya kijamii ili ofisi yake iweze kuchukua hatua.
Akikiri kuwa wingi wa migogoro inasababishwa na Viongozi wazembe, wavivu wabadhirifu, wala rushwa, Mhe. Makonda akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Ngarenaro, amewataka pia wakurugenzi na wakuu wa wilaya za Mkoa huo kuhakikisha wanasimamia maelekezo na maamuzi yatakayofikiwa kwenye kampeni hiyo ya Kitaifa.
Mhe. Makonda ambaye amekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, ametoa rai pia kwa wanasheria walio kwenye kampeni hiyo kutenga muda wa kusikiliza wananchi watakaowafikia kwa unyenyekevu na kuzingatia maadili ya taaluma zao katika kutimiza dhamira njema ya muasisi wa kampeni hiyo ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akisitiza umuhimu wa haki katika kujenga amani na kuchochea maendeleo ya Taifa, Mhe. Makonda pia ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Arusha ikiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU na wakuu wa idara mbalimbali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanasheria wa Samia, kwa kuhakikisha wanapata kila kinachohitajika katika kampeni hiyo ikiwemo wahusika mbalimbali watakaohitajika wakati wa usikilizaji wa mashauri ya wananchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa