Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Arusha kushirikiana kwa pamoja kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa, utovu wa maadili na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji kwenye taasisi zao.
Akizungumza na Wakuu wa vyombo hivyo mkoani Arusha pamoja na watendaji wa mamlaka zinazohusika na ulinzi wa Raia na mali zao, Mhe. Makonda amehimiza mashirikiano hayo na kutaka operesheni hiyo ya kujisafisha wenyewe ifanyike ndani ya mwezi huu wa saba.
"Najua mna taarifa za maeneo yanayolalamikiwa, tusaidiane, kwa mfano nilimuambia RPC akafanye mabadiliko kituo cha Polisi Murieti, hiki ni kituo kimoja ambacho kinalalamikiwa sana", Ameongeza Mhe. Makonda.
Aidha Mhe. Makonda amevitaka vyombo vingine vya ulinzi na usalama kushirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Arusha katika kutoa taarifa za ubadhirifu na rushwa miongoni mwao, kama sehemu ya kuitunza imani ya wananchi kwa vyombo hivyo muhimu kwa usalama wa raia na usimamizi wa sheria.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa