Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega wamefika Mkoani Arusha mapema leo Januari 06, 2024 na kuhudhuria Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha ambapo wameahidi kutekeleza kikamilifu maombi ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ya kuzijenga na kukarabati barabara za Mkoa wa Arusha ili kuchagiza uchumi wa Mkoa na kukuza sekta ya Utalii mkoani hapa.
Akiwakaribisha Mawaziri hao walioambatana na Watendaji wakuu wa Wizara zao akiwemo Katibu Mkuu wa Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour, Mhe. Makonda ameeleza kuhusu ubovu wa barabara za Arusha, akiwaomba Mawaziri hao kuharakisha ujenzi na maboresho yake kutokana na umuhimu wa barabara hizo katika kukuza uchumi na utalii wa Arusha pamoja na uthabiti kuelekea kwenye msimu wa michuano ya Kandanda ya barani Afrika (AFCON) inayotarajiwa kuchezwa Arusha, Dar Es salaam, Zanzibar kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda mnamo 2027.
Katika Maelezo yake Waziri Mwigulu ameahidi Wizara yake kuharakisha utoaji wa fedha za ujenzi na kuziweka baadhi ya barabara kwenye Bajeti ijayo ya serikali kuu huku Mhe. Ulega akiagiza kuanza mara moja kwa upembuzi wa baadhi ya barabara pamoja na kufungwa taa zinazotumia nishati jua, akisema serikali pia inatanua barabara kuu ya Bagamoyo- Arusha ili kuondoa msongamano kwa wageni na wenyeji wanaofika Arusha kutokea Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro na wote wanaotumia barabara hiyo inayounganisha nchi za jirani pamoja na mikoa ya Kaskazini na Mashariki mwa Tanzania.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa