Na Elinipa Lupembe.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, ameliaga kundi la nne awamu ya pili, lenye jumla ya kaya 118 na watu 818, kundi ambalo ni kubwa kuondoka kwa hiari, kutoka kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, zikielekea maeneo ya Msomera Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga, Kitwai Wilaya ya Simanjiro na Saunyi Wilaya ya Kilindi na maeneo mengine waliyoyachagua wenyewe.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuwaaga wananchi hao, wakiwa na mifugo yao 3,129, Mhe. Mongella amewapongeza kwa uzalendo mkubwa, waliouonyesha kwa nchi yao, kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa, bila kujali masilahi yao binafsi huku akiwahakikishia usalama wa maisha yao, kiuchumi na kijamii pamoja na kulipwa haki zao zilizoainishwa kisheri.
Ameongeza kuwa, pamoja na mikakati wa Serikali, kuendelea kutunza eneo la hifadhi ambalo ni Urithi wa Dunia, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuhakikisha Serikali inasimamia ulipwaji wa haki za msingi za wananchi walioamua kuhama kwa hiari kupisha eneo hilo.
"Dkt. Samia amehakikisha kila Kaya inayokwenda Msomera na maeneo mengine, inapata nyumba kwa ajili ya makazi, eneo la kilimo na mifugo pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za afya, maji, umeme, shule ili kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule" Ameweka wazi Mhe. Mongella.
Awali, Mhe. Mongella ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajafanya maamuzi ya kuhama eneo la hifadhi, kufanya maamuzi kwa haraka, kwa kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha wananchi hao, wanapata haki zao zote kwa wakati na kuwataka Maafisa Wahifadhi kuendelea kutoa elimu ili waweze kuhama kwa hiari.
Hata hivyo, wananchi hao wameishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa uongozi makini wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu, kwa kuwajali na kuamua kuwahamisha eneo la Hifadhi, ambalo lilikuwa ni hatarishi kwa maisha yao pia.
Sindato Ngenyike Mollel, aliyekuwa mkazi wa kata ya Nainokanoka, amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapa elimu na kuelewa umuhimu wa kupisha eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na hatimaye kuamua kuhama kwa hiari na kuelekea maeneo mengine ambayo Serikali ya awamu ya sita imewapangia.
"Sisi tumeamua kuhama kwa hiari yetu wenyewe bila kulazimishwa ili kupisha eneo la Hifadhi, zipuuzeni habari za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari, tunalazimishwa kuhama, tumeelilishwa na kuelewa umuhimu wa hifadhi yetu, ambayo ni urithi wa Dunia "
Naye Theresia Sabore Moko, amempongeza na kumshukuru Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuziandalia familia zao makazi mapya nje ya eneo Hifadhi, eneo ambalo mara kwa mara familia zao, zilijeruhiwa na wanyama, na wengine walipoteza maisha kwa kushambuliwa na wanyama.
"Mimi na familia yangu, tumeamua kujiandikisha kwa hiari, kuhamia Msomera, eneo ambalo Serikali imetupa bure bila kutoa gharama yoyote, tumeona ni eneo salama kwa maisha yetu na familia, zaidi tumeamua kuanza maisha mapya na kuanza kufanya shughuli za uzalishaji mali, shughuli ambazo tukiwa ndani ya Hifadhi hatukuruhusiwa kuzifanya kama vile kilimo" Amebainisha Theresia
Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Richard Kiiza, amefafanua kuwa, kundi hilo limefanya kufikia jumla ya Kaya 264, watu 1,853 na mifugo 6,934 kwa awamu hiyo ya pili, na kuongeza kuwa taratibu zote za malipo ya stahiki za kaya hizo yameshafanyika ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mapokezi katika maeneo yote wanayokwenda kuishi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa