Ujumbe kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi, umefanya ziara ya mafunzo, katika Mkoa wa Arusha ili kuangalia fursa za utalii wa ndani ya mkoa huo, na kujenga uelewa wa pamoja hatimaye kuweza kutumia na kuzitangaza fursa hizo kwa wadau wengine.
Akizungumza na wageni hao, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, amezitaja fursa mbalimbali za utalii, zinazopatikana nchini Tanzania hususani mkoani Arusha, na kusisitiza kuwa ni Taifa hilo lenye amani na utulivu wa kiuchumi muda wote.
Amesema kuwa, sekta ya utalii Arusha inachangiwa na mambo mtambuka, ikiwa ni pamoja na uwepo wa miundombinu rafiki za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni, zinazowezesha shuguli za utalii kufanyika muda wote, mambo ambayo yanaiweka Arusha kuendelea kuwa kama kitovu cha utalii wa Afrika.
"Uwepo wa miundombinu ya barabara zinazopitika kipindi chote cha mwaka, upanuzi wa viwanja vya ndege na huduma upatikanaji rahisi wa huduma za kijamii maji safi na salama, huduma za elimu, malazi na chakula, pamoja na uwepo wa Mahakama ya Afrika, zote ni fursa zinazochangia sekta ya utalii nchini" Amesema Mhe. Mongella
Hata hivyo kutokana na safari hiyo ya kielimu, ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, umepata uelewa wa kina wa fursa kubwa ya utalii ndani ya Tanzania na Mkoa wa Arusha hasa.
Pamoja na mambo yote, wamekiri kufanikiwa kutambua umuhimu wa utalii wa ndani, katika kukuza uchumi wa ndani, maendeleo endelevu, na uwezeshaji wa jamii katika sekta ya utalii.
Ziara hiyo ililenga kukipatia Chuo cha Taifa cha Ulinzi uzoefu wa vitendo katika nyanja ya utalii wa ndani huku kikionesha uwezo na rasilimali nyingi zilizopo ndani ya Mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa