Na. Daniel Gitaro
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella amepata wasaa wa kuzungumza na wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mlimani Muriet muhula wa masomo 2024 wakati alipotembelea shule hiyo kukagua maendeleo ya mapokezi ya wanafunzi waliopangiwa shuleni hapo.
Mhe. Mongella amewaasa wanafunzi hao kwa mambo kadha wa kadha ikiwemo kuwa na nidhamu, kufanya kazi kwa bidii huku wakimwamini Mungu katika masomo yao sambamba na kuwa na malengo.
Aidha amewataka viongozi maafisa Elimu pamoja na Watendaji wa Vijiji na Kata kuendelea kuwahamasisha wazazi kuwaandikisha watoto waliofika umri wa kuanza shule kwa kuwa Serikali imeshafanya sehemu yake ya kuandaa mazingira bora kwa ajili ya watoto wa Kitanzania kupata Elimu.
“Serikali imekwisha tekeleza majukumu yake ya kuleta fedha zilizotekeleza ujenzi wa miundombinu rafiki kwaajilli ya watoto kupata elimu iliyo bora, viongozi sasa ni wajibu wetu kuhamasisha wazazi kuwaandikisha watoto waliofika umri wa kuanza shule.” Amesema Mhe. Mongella.
Hata hivyo, ametoa rai kwa viongozi wa Jiji la Arusha kuongeza umakini katika kusimamia utekelezaji wa miradi katika viwango vinavyostahili kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi za kutekeleza miradi hiyo.
Aidha, wanafunzi hao, licha ya kumshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuwatembelea na kuwatia moyo katika safari hiyo mpya ya masomo waliyoianza, wameishukuru Serikali kwa kuwaandalia mazingira bora ya ujifunzaji yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kazi kubwa na kutujengea shule nzuri yenye walimu wazuri, tunaahidi kusoma kwa bidii na kufaulu.” Amesema Noel Emmanuel, Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mlimani Muriet.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Beatrice Gregori Tarimo ameahidi kuendelea kusimamia taaluma kwenye shule hiyo sambamba na miradi itakayoendelea kutekelezwa shuleni hapo ili kufikia malengo ya Serikali.
Awali, shule hiyo ilipangiwa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 200 na hadi sasa wanafunzi walioripoti ni 177, wavulana ni 84 huku wasichana wakiwa ni 93.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa