Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amezindua chanjo ya UVIKO 19 kwa Mkoa wa Arusha na kuwataka wananchi wasiwe na hofu ya kukosa chanjo.
Amesema chanjo ipo na itawatosha wale wote wenye sifa ya kuchanjwa na kwa sasa kipaombele ni wenye magonjwa nyemelezi, watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 na watumishi wa sekta ya afya.
"Ondoeni hofu ya kukosa chanjo kwani ipo ya kutosha na kila anaestahili kuchanjwa atachanjwa".
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwa makundi ya watu wanaostahili kuanza kuchanjwa.
Mongella amesema Arusha kama kitovu cha Utalii itapendeza na kila wananchi apate chanjo ili kuwatia Moyo watalii wa nje kwani wataona tupo salama.
Nae, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia amesema Dunia kwa sasa ni kama Kijiji na mwingiliano ni mkubwa hivyo amewasihi wananchi wa Arusha kutokuogopa hiyo chanjo.
Dkt. Kihamia amesisitiza kuwa kuna watu wanasafiri ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza mwingiliano wa watu na bila kuchanjwa wanakuwa hawako salama sana katika mazingira hayo.
Kila atakaechanjwa ahakikishe anaendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na UVIKO 19 ili kujiweka salama zaidi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Gofrey Pinda, amewataka watu wote waliochanjwa kwenda kuwa mabalozi wazuri katika Jamii zao ili wahamasishe Jamii yao kuchanjwa pia.
Amesema kikubwa wananchi wanatakiwa kuelewa umuhimu wa chanjo kwanza kabla ya kuipinga.
Mhe. Pinda amewaomba wananchi wa Arusha wachangamkie fursa hiyo ya kuchanjwa kwani itafika muda hawataipata chanjo kirahisi.
Uzinduzi wa chanjo ya UVIKO 19 kwa Mkoa wa Arusha umefanyika leo Agosti 3, 2021 kwa Wilaya zote Saba na jumla ya chanjo 50,000 zimepokelewa katika Mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa