Sekta zote Mtambuka katika Mkoa wa Arusha zimetakiwa kutenga bajeti katika mipango yao ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kama inavyoelekezwa kwenye Mwongozo wa Taifa.
Agizo hilo limetolewa na Kaimu Afisa ELimu Mkoa wa Arusha, Emmanuel Maundo wakati akifungua kikao cha tathimini ya Programu hiyo, kilichowakutanisha wadau mbalimbali kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Afisa ELimu huyo, amesema kuwa PJT-MMMAM ni programu muhimu kwa maendeleo ya taifa, kwani inalenga kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata malezi, makuzi na maendeleo bora ya awali.
“Kila Sekta Mtambuka inapaswa kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata ili kutekeleza Shughuli za MMMAM sambamba na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupata matokeo yatakayoleta tija kwa jamii”. Amesisitiza.
Aidha, amesisitiza pia Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa PJT-MMMAM katika ngazi ya Mkoa, wilaya na kata, Kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli hizo Pamoja na Kufanya tafiti na tathmini za mara kwa mara ili kubaini maendeleo ya PJT-MMMAM.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Arusha Blandina Nkini, amesisitiza umuhimu wa kufanya vikao vya tathimini kila robo ili kujua changamoto zilizopo na namna bora ya kuzitatua.
Hata hivyo, Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wameeleza baadhi ya changamoto zinazoikabili program hiyo ikiwa ni Pamoja na mfumo dume miongoni mwa jamii za wilaya ya Longido na Ngorongoro mambo yanayotajwa kuchangia wazazi wa kiume kushindwa kuwajibika kikamlifu katika malezi yenye mwitikio kwa watoto wenye umri wa mwaka sifuri mpaka nane.
Awali, kikao cha taarifa utekelezaji wa programu jumuishi ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT_MMMAM) cha halmashauri zote Mkoa wa Arusha kinajadili utekelezaji wa programu hiyo kwa robo ya tatu ya mwaka 2024
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa