Na Elinipa Lupembe
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania hususani katika sekta ya Utalii ili kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya nchi.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa msimu wa tisa wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu - Kili Fair 2024 mkoani Arusha, Waziri Kairuki amesema kuwa, vivutio mbalimbali vimeendelea kuwekwa na Serikali chini ya Mheshimiwa Rais ,Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha sekta binafsi inafanya kazi zake bila ya vikwazo katiba kuimarisha utalii nchini.
Aidha, Mhe. Kairuki amebainisha kuwa maonesho ya msimu wa 9 ya mwaka 2024, yamekuwa na mafanikio makubwa kuliko miaka iliyopita kutokana na kuwa na washiriki takribani Makampuni ya Utaklii 460 yakishiriki ikilinganishwa na makampuni 400 yaliyoshiriki mwaka 2023.
"Niwaponhezee waandaji na washiriki zaidi ninaishukuru Serikali ya Mkoa wa Arusha inayoongizwa na Mhe. Paul Christian Makonda pamoja na wadau wengine wa Utalii wa ndani na nje ya nchi, kwa kufanikisha maonesho haya makubwa ya utalii kwa ukanda wa Afrika Mashariki, mmefanya kazi nzuri yenye mafanikio makubwa kwa Taifa na Dunia". Amesema Mhe. Kairuki.
Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yamezinduliwa Juni 07, 2024 kwenye viwanja vya Magereza Kisongo huku makampuni 460 yakishiriki, maonesho ambayo hufanyika kila mwaka kwa siku tatu mfululizo yakiwa na lengo la kukutanisha wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania ili kubadilishana bidhaa, taarifa na uzoefu unaotokana na sekta ya utalii.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa