Na Elinipa Lupembe.
Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB, imejipanga kumuwezesha mfugaji wa ng'ombe wa maziwa Bi. Teddy James, wa kata ya Sombetini Jiji la Arusha, kwa kumpatia fedha kwa ajili ya kununu eneo kubwa la malisho pamoja na kumjengea uwezo wa kukuza mtaji wa biashara hiyo ya ufugaji.
Akizungumza mara baada ya kumtembelea mfugaji huyo na kujionea hali halisi ya ufugaji bora anaoufanya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, licha ya kuridhishwa na kufurahishwa na kazi kubwa anayoifanya mfugaji huyo, amekiri kumuunga mkono, kwa kusimamia upatikanaji wa eneo kubwa kwa ajili ya malisho pamoja na upatikanaji wa fedha kupitia benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB.
Mhe. Mongella amemsifia na kumpongeza mfugaji huyo, kwa mradi mzuri wa ufugaji wa kisasa anaoufanya katika eneo dogo la mjini, huku akiahidi kuendelea kumsimamia
na kuhakikisha, anapata eneo kubwa kwa ajili ya kupanua shughuli hizo za ufugaji sambamba na kuhakikisha benki ya TADB inampatia fedha kwa ajili kununua eneo na kukuza mtaji wa biashara yake.
"Inafurahisha sana kwa mtanzania kama Teddy, anafanya biashara kubwa kama hii ya ufugaji wa kisasa, biashara ambayo kama Serikali tutamuunga mkono, ili aifanya kwa ukubwa zaidi na kupanua soko la ndani na nje ya nchi, licha Teddy kufanya ufugaji wa kisasa lakini anafanya biashara ya kuuza maziwa zaidi ya lita 1000 kwa siku kuuza mitamba na ng'ombe wakubwa kwa wafugaji wengine, kama Serikali ya Mkoa, ninaahidi kusimamia ukuzaji wa mtaji wake" Amesisitiza Mhe. Mongella
Aidha, ameweka wazi kuwa, asili ya wenyeji wa Mkoa wa Arusha ni wafugaji, wanohitaji kuendana na mabadiliko ya maendeleo ya dunia, kwa kufanya ufugaji wa kisasa kama ilivyo kwa Teddy, Serikali inahitaji watanzania wajasiriamali wa mifugo wengi zaidi.
Hata hivyo, Mhe. Mongella ameweka wazi kuwa, tayari benki ya Kilimo, iko kwenye hatua za mwisho za kumpa mkopo, ili kukuza mtaji na kuongeza uzalishaji, huku Mkoa ukiendelea kumpa ushirikiano na utalaam ili mfugaji huyo aendelee kukua zaidi.
Naye Bi Teddy James, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kuwawezesha watanzania hususani wafugaji kwa kuwa na programu za kutoa fedha nyingi ili kuwainua, amesema kuwa, tayari Benki ya TADB, imeridhia kumpa fedha ili aweze kununua eneo pamoja na kukuza mtaji na kuongeza uzalishaji kwenye biashara yake ya ufugaji.
"Ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa mama Samia, binafsi ninamuunga mkono kupita kauli yake ya Kazi Iendelee, ninafuga ng'ombe zaidi ya 120 na kupata maziwa lita 1000 kwa siku, ambayo ninahudumia kiwanda cha maziwa cha Kilimanjari Fresh, ninauza mitamba na ng'ombe wakubwa kwa wafugaji wanaohitaji ng'ombe bora wa maziwa" Amesema Teddy
Awali, mtoto wa mfugaji huyo, mwenye shahada ya Biashara na Uhasibu, CPA. Mariamu, amesema ameamua kuachana na swala kufuta ajira serikalini, na kujikita kwenye ufugaji huku akiwasisitiza vijana wengi kujiajiri na sio kutegemea ajira kutoka serikalini pekee.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa