OR - TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha Maslahi ya Walimu ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba za Makazi kwenye vituo vyao vya kazi ili kuwawekea mazingira nadhifu ya kazi.
Mhe. Rais amesema hayo leo Disemba 17, 2023 wakati akiongea na Jumuiya ya Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) kwa njia ya Simu wakati wa Mkutano uliowakutanisha zaidi ya wajumbe 3500 kwenye Ukumbi wa Kwatunza Beach Resort Mkoani Mwanza wakati Waziri wa TAMISEMI akifunga Mkutano huo wa 18 wa Mwaka.
"Serikali ina imani sana na Walimu nchini na kwakweli tupo tayari kuboresha mazingira yenu ya Kazi na katika kutekeleza hilo tunalifanyia kazi suala la Maslahi yenu katika mambo mbalimbali na kwenye Bajeti ya Mwakani tunakwenda kujenga nyumba nyingi za Walimu pamoja na kuboresha Maslahi yenu." Amesemq Rais Samia.
Akizungumza na walimu hao, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Mb) Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka kwenda kushirikiana na wazazi na viongozi kuhakikisha wanafunzi wanajiunga na Masomo ifikapo Januari 08, 2024 wakati wa kuanza kwa Muhula wa Masomo bila kuchelewa.
Amebainisha kuwa kumekua na ongezeko la Ufaulu kwa watahiniwa wa Darasa la Saba hadi 1.57% ukilinganisha na mwaka 2022 hadi kupelekea wanafunzi 1,092,984 waliofaulu Mitihani ya Darasa la Saba kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza katika Shule mbalimbali za Sekondari nchini 2024 hivyo ni lazima waenzi hali hiyo isishuke bali ipande.
Halikadhalika, amewataka watendaji ngazi zote kwenye Halmashauri na Mikoa kuhakikisha ifikapo Disemba 31, 2023 miradi yote ya Elimu iwe imekamilika ili kuwapa mazingira bora ya wanafunzuli kusoma na kwa Mkurugenzi ambaye hatafanya hivyo basi hatosita kumsimamisha ili aondolewe kwenye madaraka yao.
Rais wa TAHOSSA ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Ilboru Sekondari Denis Otieno amesema humuiya hiyo imejidhatiti katika kusimamia ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa mujibu wa miongozo iliyopo, kuthibiti utoro wa walimu na wanafunzi ili kusaidia kupandisha ufaulu pamoja na kusimamia nidhamu na maadili ya walimu shuleni.
"Kikokotoo imumekua msamiati ambao wastaafu wengi umekua ukiwaumiza si tu baada ya kuondoka kazini bali hata wakati wakikaribia kuondoka na kwakweli Mhe. Mgeni Rasmi tunaomba ukatusaidie kufikisha ombi letu la kuona namna ya kutafuta ufumbuzi kwenye suala hili." Rais TAHOSSA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI Mhe. Denis Londo ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa Kutekeleza kwa vitendo adhma ya kuboresha Elimu nchini kwa kujenga miundombinu na kuboresha mitaala na ajira za walimu na akawataka walimu kujituma.
"Walimu ni Jeshi kubwa, hapa Mwanza mpo salama kabisa na mtakapokuja wakati mwingine mtaikuta ipo mahala pengine, tunazidi kusonga mbele kwa maendeleo na kwakweli tuna bahati sana maana miradi Mikubwa ya kimkakati ya Maendeleo nchini inafanywa Mwanza." Amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CPA Amos Makalla.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa