Shamba lenye ukubwa wa ekari 43.5 lililokiwa likimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations limekabidhiwa rasmi kwa Serikali kwa ajili ya kuliendeleza zaidi.
Makabidhiano ya shamba hilo yamefanyika katika Kijiji cha Bwawani kata ya Bwawani ndani ya Halmashauri ya Arusha.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Waziri wa ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula amesema, makabidhiano hayo yamefikiwa baada ya mwekezaji huyo kutoka Kampuni ya Tanzania Plantations kukiuka masharti ya uwekezaji mnamo mwaka 1999.
Waziri Mabula amesema, maamuzi hayo ya kulirudisha shamba hilo chini ya Serikali ni kwa manufaa ya Serikali na wananchi hasa wa eneo hilo.
Amesisitiza zaidi kwa wananchi wa Kijiji cha Bwawani kuwa na subira ya kusubiri Serikali inaweka mpango mzuri wa matumizi ya ardhi hiyo,hivyo wasifanye shughuli zozote katika shamba hilo hadi utaratibu huo utakapokamilika.
Mhe.Mabula amesema, mpango wa matumizi bora ya shamba hilo utafanyika ndani ya miezi 3 tu na wakazi wa eneo hilo ndio watapewa kipaombele.
Aidha amesema hatua za mpango wa matumizi ya shamba hilo utakuwa shirikishi na wananchi wa eneo hilo watashirikishwa kwa ukaribu zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amewataka wananchi wa Kijiji hicho kutogeuza shamba hilo kama shamba la Bibi kwa kutaka kufaidi zaidi.
Pia amewataka viongozi wa Kijiji na Kata kutopata ushawishi na kuleta watu kutoka nje ya Kijiji hicho ili nao waweze kunufaika na shamba hilo.
Aidha, amemuakikishia Waziri kuwa zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya shamba hilo utafanyika kwa haraka na kwa muda uliopangwa na wananchi watahusika kwa kiwango kikubwa.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amesema Kampuni ya Tanzania Plantations imelipwa jumla ya Bilioni 5.7 na Serikali baada ya Kampuni hiyo kufungua mashauri dhidi ya Serikali kwa kuvunja mkataba wa umiliki wakati Kampuni hiyo ilishawekeza mali nyingi kama Nyumba na mashine za kutengeneza katani.
Amesema mnamo mwaka 2015 Kampuni hiyo iliamua kuondoa shauri hilo mahakamani na makubalino ya malipo ya fedha hizo yakafanyika nje ya Mahakama na Serikali haidaiwi na Kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Plantations Bwana Pradip Lodhia ameishukuru Serikali kwa kumaliza shauri hilo kwa amani na amefurahi kukabidhi shamba hilo kwa Serikali.
Nae, Diwani wa Kata ya Bwawani Justine Rengatia ameiomba Serikali itakapoamua kuwauzia shamba wananchi wa Kijiji hicho basi wapewe muda wa kulipa kwa awamu kutokana na hali ya uchumi wao kuwa duni.
Mgogoro wa shamba hilo umedumu zaidi ya miaka 20 na ulikuwa kati ya Serikali na aliyekuwa mmiliki wa shamba hilo kampuni ya Tanzania Plantations na umemalizwa mnamo mwaka 2022.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa