Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amewataka wasimamizi wa mizani inayosomamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutenda haki kwa wasafirishaji hasa wanapokutwa na makosa ya kuzidisha uzito.
Waziri Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Arusha wakati wa sherehe ya ufunguzi wa mizani ya kisasa ya Kimokouwa uliopo wilayani Longido ambayo itatumika kwa ajili ya kupima uzito wa magari yanayofanya safari zake kati ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya.
“Sheria inayosimamia mizani ya Afrika Mashariki ni kali sana na ina tozo kubwa hivyo hakikisheni mizani zinakuwa katika vipimo sahihi ili kuondoa mkanganyiko wa uwiano za mizani unaojitokeza mara kwa mara”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amekema vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya wasimamizi wa mizani kwani athari ya kumuandikia msafirishaji tozo ni kubwa na nyingine zinagharimu zaidi ya gharama ya gari husika.
“Angalieni namna bora ya kuelemisha kwani unakuta gharama ya tozo ni kubwa kuliko hata thamani ya gari husika na kwa mujibu wa sheria lazima itozwe tozo” amefafanua Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa ametoa agizo kwa TANROADS kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu za mara kwa mara kwa watumishi wa mizani, wasafirishaji na madereva kuhusu sheria ya mizani na pamoja na kufanya tafiti kujua tatizo la kutokuwa na uwiano sawa wa uzito wa gari kutoka mizani moja hadi nyingine.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila, amesema kuwa mizani hiyo inayopima magari pande zote mbili za barabara umegharimiwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 14.7.
Ameeleza kuwa mradi huo upo katika barabara kuu ya Arusha – Namanga ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kimataifa inayojulikana kwa jina la The Great North Corridor ambapo mtu anaweza kusafiri kutoka Cairo, Misri kupitia Nairobi – Arusha – Babati – Dodoma – Iringa – Tunduma hadi Cape town, Afrika ya Kusini.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mizani huo kutaondoa ucheleweshaji wa magari wakati wa upimaji uzito pamoja na kupunguza muda wa kusafiri hasa kwa magari ya mizigo yanayokwenda au kutoka nje ya nchi na kuongeza uwazi katika utendaji kazi na hivyo kupunguza malalamiko kutoka kwa wadau wa usafirishaji.
Eng. Mativila ameeleza kuwa mradi huo umejengwa na kampuni ya CRJE (East Africa) na kusimamiwa na Ambicon ya Dar es Salaam.
Mizani ya Kimokouwa ilianza kujengwa mnamo tarehe 11 Mei 2020 kwa lengo la kudhibiti uzidishaji uzito wa magari yanayotumia barabara Kuu ya Arusha-Namanga ili kuwezesha miundombinu ya barabara kudumu kwa muda uliokusudiwa wakati wa usanifu wake.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa