Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) imekutana na wadau wa sekta binafsi mkoa wa Arusha na kufanya kikao kazi kwa lengo la kukusanya maoni na mapendekezo kuhusu vipaumbele na mikakati ya maendeleo, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kikao kazi hicho chenye lengo kuu ni kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kubainisha maeneo ya kipaumbele, ubia, na mikakati itakayowezesha kufikia malengo ya Dira hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha mapema leo Oktoba 09,2025.
Aidha, Tume hiyo inalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi juu ya wajibu wa kila upande katika utekelezaji wa Dira 2050, sambamba na kuweka msingi imara wa maandalizi ya mpango mkakati wa ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.
Uratibu wa kikao hiki unatokana na jukumu la kisheria la Tume ya Taifa ya Mipango la kuratibu ushiriki wa sekta binafsi katika maandalizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini. Baada ya uzinduzi rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tume imeanza mchakato wa kuweka mikakati ya utekelezaji wake, ambapo ushirikishwaji wa sekta binafsi ni sehemu muhimu katika kuhakikisha Dira hii inatekelezeka kwa ufanisi, uendelevu na tija kwa wananchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa