Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Filipo Isidory Mpango amemwagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kukaa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha(AUWSA) ili Mamlaka hiyo kujifunza Teknolojia ya Kisasa ya kutumia Maji taka katika umwagiliaji mashamba toka Nchi ya Israel.
Hayo ameyasema leo wakati akikagua Mradi wa kutibu Maji taka katika Jiji la Arusha ulio chini ya AUWSA kwa vile mradi huu ukitumika vizuri utakuwa na fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa Kata ya Terrat kwa kutumia Kilimo cha Umwagiliaji na kuwataka kuuitunza mradi huo.
"Maji taka haya yakisafishwa vizuri yanauwezo wa kutumika tena kwajili ya shughuli za Kilimo cha Umwagiliaji,ufugaji samaki na upandwaji miti utakaosaidia katika miradi ya ufugaji nyuki" alisema Dkt Mpango.
Akitoa taarifa ya Mradi huo kwa Makamu wa Rais;Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka na Usafi wa Mazingira Mhandisi Justine Lujomba amesema Mradi huo wa ujenzi wa Mabwawa una thamani ya Bilioni 39.8 na una mabwawa 18 yakiyokamilika ikiwa ni sehemu ya Mradi mkubwa wa ujenzi na usambazaji maji Jiji la Arusha na viunga vyake wenye thamani ya shilingi bilioni 520.
Mhandisi Justine Lujomba amesema fedha hizo zimetoka kwa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB) na kuwa mabwawa hayo yamesaidia kutibu maji taka takribani lita 22,000,000/= kwa siku ikilinganishwa na lita 3,500,000/= zilizokuwa zikichakatwa kwenye mabwawa ya awali.
Aidha,Mhandisi Lujomba amesema faida kubwa ya waliyoipata kutokana na uwepo wa mradi huo ni pamoja na kuongozeka kwa wateja waliunganishwa katika mtandao huo na kufanya Jiji kuwa katika Mazingira safi.
Makamu Rais yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya Siku moja ambapo pia alifungua Kongamano la Idhaa ya Kiswahili Duniani lililofanyika katika Kituo Cha Mikutano cha Kimataifa Arusha( AICC).
MWISHO
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa