Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Hassan Kimanta amewashauri waendasha pikipiki, bajaji, daladala na machinga kujiunga na mifuko ya bima kwa ajili ya usalama wa vyombo vyao vya usafiri, biashara zao na afya.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua jengo la ofisi ya chama cha waendesha pikipiki,bajaji, daladala na wamachinga (UBOBACHIDA).
“Jiungeni na mifuko ya bima itawasaidia sana katika vyombo vyenu vya usafiri,biashara na hata pia afya zenu”.
Amesema bima ni muhimu kwao kwani wakati wowote mtu anaweza kupatwa na matatizo na bima ikatumika kusaidia katika gharama.
Aidha, amewasisitiza wanachama hao kutokukubali kutumika katika mambo binafsi ya mtu ambayo itawapelekea kuvurugana.
Umoja huo utawasaidia sana hasa kupata mikopo katika mabenki mbalimbali na hata mikopo ya serikali itakayowasaidia kuanzisha biashara mbalimbali za kuwaongezea vipato.
Akisoma risala kwa niaba ya wanachama wa umoja huo katibu wa chama bwana Ramadhani Kambelenjo, amesema lengo kubwa la umoja huo ni kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja.
Pia,umoja huo utawawezesha kutatua changamoto zao wenyewe chini ya viongozi wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina Msaidizi Salum Hamduni, amewataka madereva hao kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za barabarani.
Pia, amewataka kushirikiana bega kwa bega na jeshi la polisi Mkoa kwa kutoa taarifa zozote za uharifu huku nao akiwashauri kutoshiriki katika vitendo vyovyote vya uharifu.
Chama cha UBOBACHIDA kimeanzishwa mahususi kwa lengo la kuwaunganisha madereva pikipiki,daladala, bajaji na wamachinga kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kwa umoja.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa