Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kuwa, unahitajika ufadhili unaoweza kufikia uendelevu, wenye uwiano kati ya kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Septemba 02, 2024.
Amesema kuwa, nchi zinazoendelea zinahitaji zaidi ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia azma ya kupunguza, kudhibiti ili kupata suluhisho la kudumu kwa kuzingatia jinsia katika ufadhili huo.
Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa 35, kufanya mijadala ya kina, kubadilishana uzoefu katika mafanikio, changamoto na mafunzo ili kuweza kupata suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ufadhili unaozingatia jinsia.
Amesema kwa kuunganisha maarifa na utaalamu wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutawezesha kuongeza juhudi za kitaifa na kimataifa na kuharakisha maendeleo katika kufikia malengo ya pamoja ya ufadhili endelevu wa mabadiliko ya tabianchi unaozingatia jinsia.
Makamu wa Rais amesema mkutano huo unapaswa kusaidia katika kuhakikisha ahadi za nchi zilizoendelea za utoaji wa dola milioni 100 kila mwaka zinatimizwa ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya ahadi za nchi hizo za kuwezesha utekelezaji wa mkataba wa Paris.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa