Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, amepongeza jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini, akisisitiza kuwa mafanikio yanayoonekana sasa ni matokeo ya uongozi thabiti chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 25 Aprili 2025, alipotembelea na kukagua mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Meru, mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani huo kuelekea miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kupongeza namna fedha za umma zilivyotumika kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa huduma bora kama hizo ni matokeo ya mipango madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita.
“Huduma bora namna hii siyo bahati mbaya, ni matokeo ya uongozi makini na maono ya mbali ya Rais Samia. Hapa tumeona ubora ukizingatiwa sambamba na thamani ya fedha zilizotumika”. Amesema.
Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kuwanufaisha Watanzania kwa muda mrefu na kutoa wito kwa wananchi kudumisha mshikamano wa kitaifa kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliouasisi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema kuwa Serikali ya Mkoa imeandaa mkakati wa kuimarisha huduma za afya kwa kuanzisha ushirikiano na madaktari bingwa wa magonjwa maalum kutoka ndani na nje ya nchi kama vile Hispania.
“Tunalenga kuwa na hospitali moja maalum ya rufaa itakayoshirikiana na madaktari bingwa wa muda mrefu kutoka nje, ili kutoa huduma bora kwa wananchi wetu hasa wale wa kipato cha chini, na pia kuwa kituo cha huduma za afya kwa wageni kutoka mataifa mengine.” Amesema Mhe. Makonda.
Awali, mradi huo umetekelezwa kwa 'force account' kwa gharama ya shilingi milioni 900 zilizotolewa na Serikali Kuu, na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 100, hivyo kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa