Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia amemteuwa Katibu Tawala msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mali bwana Hargeney Reginald Chitukuro kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa muda hadi apo Serikali itakapotoa utaratibu mwingine.
Katika kikao maalumu cha kumtambulisha Kaimu Mkurugenzi huyo Dkt.Kihamia amewataka wakuu wa idara Jiji la Arusha kushirikiana nae katika kutekeleza majukumu yake.
Pia,amewataka watumishi wa Jiji la Arusha kufanya kazi kwa ushirikiano na wasikubali kupelekeshwa katika kutekeleza majukumu yao.
Dkt.Kihamia amesisitiza makabidhiano ya ofisi ya Mkurugenzi yafanyike mapema iwezekanavyo ili majukumu mengine yaendelee katika ofisi hiyo.
Ofisi ya Rais TAMISEMI ilikasimisha madarasa hayo kwa Katibu Tawala Mkoa ya kumteuwa atakae Kaimu nafasi hiyo kwa muda.
Nae, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo Bwana Hargeney Chitukuro amesisitiza kuwa na ushirikiano kutoka ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri.
Amesema, jukumu la kutekeleza majukumu yaliyopo nikufuata sheria na taratibu zilizopo ili kukuza ufanisi zaidi.
Mastahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iranghe amemuaidi Kaimu Mkurugenzi huyo ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake na kuleta maendeleo katika Jiji hilo.
Hatua ya kumteuwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha imefikiwa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo Dkt. John Pima kusimamishwa kazi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa tuhuma za ubadhilifu na amatumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa