Na Elinipa Lupembe
Viongozi wawakilishi wa wananchi wakiwemo wenyeviti wa vitongoji, vijiji, mitaa na kata, wamesisitizwa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao, ili kuhakikisha fedha zilinazotolewa na Serikali zinatumika kulingana na malengo pamoja na kuilinda, kulinda na kuithamini miradi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, alipotembelea na kukagua hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma kwenye Kituo cha Afya Mareu, Kata ya King'ori Wilaya ya Arumeru, na kukerwa na ucheleweshwaji wa matumizi ya fedha Sh. milioni 150, zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, kwenye kituo hicho.
Mhe. Mongella amewasisitiza viongozi wote na wananchi kushirikia katika hatua zote za utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yao, kufuatilia hali ya ucheleweshwaji wa miradi ili kukamilika kwa wakati huku Serikali ilihali imetoa fedha za kukamilisha mradi husika.
Amewataka viongozi hao, kufanya ufuatiliaji wa mapokezi ya fedha katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kufahamu kiasi halisi cha fedha kilichotolewa na Serikali muda sambamba na utekelezaji wa mradi hadi kukamilika pamja na thamani ya mradi mzima.
"Nyinyi Wenyeviti wa vijiji, Madiwani na Wabunge fuatilieni matumizi ya fedha za miradi katika maeneo yenu, msiwaachie watalamu peke yao kwa kuwa miradi hii ni yenu, jukumu la kuisimamia ni lenu kama viongozi" Amesisitiza Mhe. Mongella.
Hata hivyo, Mhe. Mongella, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, kufuatilia Sh.milioni 150, na kuhakikisha dawa na vifaa tiba zinanunuliwa kama ilivyokuwa maelekezo ya Serikali.
Pia alisisitiza kuwa samani zote za kituo hicho ziwe zimepatikana ikiwemo vitanda vya wagonjwa, samani za ofisi, Jenereta pamoja na kukamilisha ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji.
Naye Diwani wa Kata ya King'ori Mhe. Lucas Kaaya, licha ya changamoto hizo, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa kuwapa fedha nyingi za kutekeleza miradi katika kata hiyo, ikiwamo miradi ya afya, elimu, majina miundombinu na barabara miradi ambayo imeamsha ari ya maendeleo katika kata hiyo tofauti na awamu zilizotangulia.
Aidha alisema kuwa, wakati wa utekelezaji wa mradi huo, hakukuwa na maelewano mazuri baina ya viongozi na watalamu lakini kwa sasa wameshawekana sawa mambo yameanza kwenda vizuri huku akiahidi kushirikiana na watalamu kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji Oldonyong'iru, Mhe. Timoth Paul Lihuni, amesema kuwa, tangu uongozi wa kituo hicho kubadilishwa kwa sasa, wananchi wameanza kufurahia huduma katika kituo hicho ikiwemo huduma ya upasuaji huku akiweka wazi kuwa hapo awali hawakushirikishwa.
Kituo hicho cha afya kimejengwa na serikali kwa gharama ya shilingi milioni 500 pamoja na milioni 150 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa