Familia zilizoathirika kufuatia maporomoko ya matope yaliyotokea wilaya ya Hanan'g eneo la Kateshi mkoani Manyara, maafa yaliyotokea Desemba, 2023, na kusababisha baadhi ya watu 700 kukosa makazi, wamekabidhiwa nyumba za kuishi na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo, Desemba 20, 2024 kwenye kitongoji cha Waret.
Mhe.Majaliwa amekabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maafa hayo na akisisitiza kuwa hiyo ni ishara ya upendo na kujali kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi na kuzindua nyumba hizo, Waziri Mkuu amesema kuwa Mhe. Rais ametoa pole kwa waathirika wote na amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili waweze kurejesha mfumo wa maisha yao kama ilivyokuwa awali.
"Ujenzi wa nyumba 73 kati ya 109 umegharamiwa na Serikali Kuu na kujengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT), nyumba nyingine 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania huku nyumba moja ikijengwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UWT)" amebainisha.
Ameongeza kuwa, kufuatia maafa hayo, nyumba 109 zilihitaji kujengwa upya kwa haraka kwa kuzingatia athari hizo, na kwa upendo wake, Mhe. Rais alitoa maelekezo ya kujenga nyumba bora na za kudumu katika eneo salama kwa waathirika waliopoteza makazi yao na kusisitiza kuwa, ujenzi huu ni ishara ya kujali, upendo na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa pamoja na wananchi hususani wakati wa shida.
Hata hivyo, Mhe Rais Dkt. Samia alitoa fedha, kiasi cha shilingi Bilioni 1.38 kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii ikiwemo umeme, maji na barabara za uhakika, kwa lengo la kuhakikisha kila nyumba inafikiwa na huduma hizo muhimu.
Awali, Mhe.Majaliwa amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanan'g, kuratibu zoezi la ugawaji wa viwanja vya ziada vilivyopo katika eneo hilo ili kuendeleza eneo hilo liwe na wakazi mchanganyiko sio wale walioathirika peke yao.
“Tunataka eneo hili lisitambuliwe kama makazi ya waathirika, bali kijiji rasmi chenye huduma zote muhimu za kijamii na liwe kielelezo cha maboresho ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa