Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amekabidhi kiasi cha shilingi Milioni 11 kwa vituo vya kulelea watoto yatima na kwa Bw. Allan Shomari, mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu aliyewahi kuchezea timu za General Tyre na Yanga.
Makabidhiano ya vituo vya watoto yatima yamefanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa ambapo Kituo cha watoto yatima kinachosimamiwa na Msikiti wa Masjid Senta kimepatiwa shilingi Milioni 5 na kituo cha watoto walemavu kilicho chini ya Kanisa Katoliki Monduli(St.John Paul Rehabilitation Center) kimepatiwa shilingi Milioni 5.
Mhe. Mkuu wa Mkoa alifika pia nyumbani kwa mchezaji wa zamani wa Yanga, Bw. Allan Shomari na kumkabidhi shilingi Milioni Mhe. Kimanta aliahidi pia kutoa mchango binafsi wa shilingi laki 5 kwa Bw. Allan Shomari.
Mhe. Kimanta amesema fedha hizo alizokabidhi zimetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapato yaliyopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Hisani kati ya timu za Simba na Namungo iliyochezwa Jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid tarehe 30 Agosti, 2020.
Mhe. Kimanta ameviasa vituo hivyo vya watoto kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa maendeleo ya vituo vyao na si vinginevyo.
Mhe. Kimanta ameishukuru TFF kwa mchango huo wa kuwasaidia watoto wa vituo hivyo na kwa msaada walitoa kwa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Timu ya Yanga, Bw. Allan Shomari.
Mhe. Kimanta ametoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kuvisaidia vituo vya watoto yatima na wenye ulemavu na pia kujitokeza kumsaidia Bw. Allan Shomari ambaye ni mlemavu wa macho.
Akizungumza kwa niaba ya TFF, Mwenyekiti wa TFF Mkoa wa Arusha Bw. Zakayo Mjema amesema fedha hizo zimetolewa kwa vituo vya watoto yatima kama mchango wa TFF kwa jamii na ni imani yake kuwa vituo hivyo vinaweza kuzalisha wachezaji wazuri wa baadae kwa manufaa ya Taifa letu.
Bw. Mjema ameongeza pia kuwa michezo ina fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa vijana na wao kama TFF Mkoa wa Arusha wataendelea kutoa misaada kwa watoto hao ikiwemo kuwapatia mipira ya kuchezea.
Ametoa wito kwa wadau wengine kuwasaidia wachezaji wa zamani kama walichofanya kwa Bw. Allan Shomari kwa vile bado wapo wengi mitaani wanaohitaji msaada kama huo.
Akitoa neno la shukrani, Bw. Allan Shomari ameushukuru uongozi wa TFF na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Kimanta kwa msaada huo waliomkabidhi ambao utamsaidia hasa kwenye matibabu yake ya Macho.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa