Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewataka Watumishi na Viongozi wa Mamlaka za hifadhi za Taifa zilizopo Mkoani Arusha kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa uzalendo, wakitambua kuwa wanayo dhamana kubwa ya kulinda rasilimali za nchi na uendelevu wa Vivutio vya Utalii vilivyopo Arusha.
CPA Makalla ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 20, 2025 Mto wa Mbu Karatu kwenye Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, alipokutana na kuzungumza na Menejimenti ya Shirika la hifadhi ya Taifa TANAPA, akiwataka pia kuwa Mabalozi wazuri wa kusukuma mbele jitihada za Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii wa Mkoa wa Arusha na Tanzania.
"Nyie ni mabalozi wetu wazuri na tunawaamini, hakikisheni mnalinda hifadhi tulizonazo, mkitimiza majukumu yenu kwa uadilifu na uzalendo kwa nchi yenu. Utalii ni matokeo ya uhifadhi, tuunge Mkono jitihada za Mhe. Rais ambazo zimetusaidia kuwa na Ongezeko kubwa la Idadi ya watalii kwenye Hifadhi tulizonazo." Amesema Mhe. Makalla.
Aidha kando ya kusisitiza usimamizi wa sheria na Mipaka ya hifadhi kwa uadilifu na uzalendo Mkubwa, CPA Makalla pia ameahidi ushirikiano kwa wahifadhi hao, akibainisha pia umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi na utalii pamoja na kuendeleza mahusiano mema na jamii zinazozunguka hifadhi za Utalii zilizopo kwenye Mkoa wa Arusha.
Awali katika maelezo yao, Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Yustina Kiwango na Witness Shoo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha wameeleza kuongezeka kwa Idadi ya watalii kwenye hifadhi zao, suala lililoongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha, wakisema tija hiyo imepatikana zaidi kutokana na filamu za The Royal Tour na Amaizing Tanzania, zilizoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa